KAMA UNAPENDA KUISHI NA FURAHA MWAKA HUU 2016 FANYA MAMBO HAYA MATANO MUHIMU

Ikiwa leo ni Januari 04, 2016 mwaka ndio kwanza unaanza kabisa nimeona ni vyema tufahamishane haya mambo ya msingi yatakayokusaidia kuishi ukiwa na furaha ndani ya mwaka huu.


Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiishi pasipo kuwa na furaha kwa muda mrefu kutokana na sababu za kimaisha pamoja na magumu wanayoyapitia katika mazingira yao ya kila siku.

Ni wazi kwamba katika maisha kuna wakati huwa tunajikuta tunapitia mambo magumu, ambayo mara nyingine hupelekea hata kukata tamaa kabisa na kujikuta ukiishi bila kuwa na furaha kabisa, hata hivyo wataalam wa mambo ya saikolojia wanasema tatizo hili huweza kutatulika kwa kuanza na mhusika mwenyewe anayepitia katika hali hiyo.

Inaaminika kuwa furaha hutegemea sana na wewe mwenyewe mhusika na wala si vitu au watu wengine, huenda unapitia katika hali hiyo kwa kipindi hita tafadhari hebu jaribu kuyazingatia haya machache kwa ajili ya kurejesha furaha yako.

Acha kuwajali wale wanaokuondolea furaha
Inawezekana kila siku huwa upo karibu na watu ambao huchangia kuondoa furaha yako na huenda umekuwa ukijaribu kuwavumilia na kujikuta unashindwa kabisa, hivyo ni vyema ukawapuuza au kama inawezekana kaa nao mbali.

Tafuta mahali pengine unapoweza kukaa kwa amani na furaha, kwa sababu hakuna haja ya kuendelea kuhuzunika kwa sababu ya mtu au watu fulani ambao wanachangia kuondosha furaha ya maisha yako.

Amua kuwa mshindi katika maisha yako sasa
Hii ni ile namna ya kujijengea uwezo na kuamini kwamba wewe ni mshindi, haijalishi ni magumu kiasi gani unapitia kwa sasa. Hakikisha siku zote unachagua kufanya mambo yako kwa uhodari na kujiamini, hata kama baadhi ya watu watakuvunja moyo au kukudharau.

Anza kuwasamehe wale waliokukosea
Msamaha ni muhimu kwa sababu hapa duniani hakuna mtu aliyekamilika na hata vitabu vya dini vinatuhamasisha kusameana pindi tunapokoseana. Inawezekana kuna mtu amekutenda kitu kibaya huenda kwa makusudi au bahati mbaya, lakini kwa ujumla wake tunasema amekukosewa.

Si vizuri kukaa au kuishi na kisirani kwa sababu ya mtu au watu waliokufanyia ubaya kwa muda mrefu, kwani huweza kukusababishia matatizo ya kiafya (depression) au kuharibu kabisa uhusiano wako na watu uliokosana nao. Kuwa na tabia ya kuyasahau maudhi unayoyapata kwa watu na inapobidi waelewe juu ya makosa yao kuliko kukaa na kisirani.

Siku zote simamia kwenye ukweli na uadilifu
Tunafahamu kwamba, wengi wetu hatupendi kudanganywa na wala sina uhakika endapo wewe unapenda kudanganywa, hivyo kama wewe hupendi kufanyiwa hivyo basi na wewe usifanye kwa wengine.

Mtu unapokuwa muadilifu na mkweli matokeo yake watu hukuamini na kukutegemea katika mambo mbalimbali jambo ambalo husaidia kuimarisha furaha ya maisha yako zaidi pia.

Penda kuwa mkarimu kwa wengine
Kumbuka si watu wote wanaweza kukuona kuwa wewe ni mwema hata utende mambo yaliyo mema maisha yako yote, hivyo jitahidi kuwa mkarimu kwa watu wote bila kujali endapo wanatambua wema wako au hawatambui. Hii husaidia kutojali na kuumia sana pale utakapoona watu hawajachukulia mchango wako kwa uzito ulioutegemea hivyo utaendelea kubaki na furaha yako muda wote.

Imeandaliwa na Tabibu Abdallaha Mandai wa Mandai Herbalist Clinic kwa maelezo zaidi au ushauri wasiliana naye kwa simu namba  0716 300 200, 0769 400 800, 0784 300 300. Barua pepe, dkmandaitz@gmail.com. Au tembelea website yake www.dkmandai.com.


No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname