FAHAMU VYAKULA AMBAVYO HUTAKIWI KULA BAADA YA KUFANYA MAZOEZI
Mazoezi ni miongoni mwa vitu vinavyosisitizwa na wataalamu wa afya kwa ustawi wa mwili wa binadamu, huku yakiwa na mchango mkubwa katika kuukinga mwili na maradhi mbalimbali.
Mwili wa binadamu ukiachilia kufuata utaratibu wa lishe iliyokamilika wataalamu wanasema kinachofuata ni mazoezi ili kuuweka fiti na kuupa nguvu ya kupambana na kila kinachokuja mbele yake.
Kwa maana hiyo pamoja na kula mlo kamili, kunywa maji kwa wingi, bado mwili unahitaji mazoezi ili kukamilisha kinga na uimara wa kujikinga na maradhi na kuwa mwenye afya njema muda wote.
Kama ilivyo ni muhimu kuyafanya , kuna vyakula pia ambavyo ni hatari kuvila saa mbili baada ya kufanya mazoezi ikiwamo vile vyenye sukari nyingi. Hatari yake ni kuharibu kile chote ulichokipata kwa kufanya mazoezi.
Tovuti ya masuala ya afya iitwayo fitness.mercola.com imebainisha kuwa kutumia vitu vya sukari saa mbili baada ya kumaliza mazoezi huharibu mfumo mzima wa ulichokifanya kwa makusudi ya kujenga mwili na badala yake huzalisha homoni bila mpangilio.
Tovuti hiyo imeeleza kuwa utumiaji wa vyakula vya sukari hata hii ya majumbani saa mbili baada ya kufanya mazoezi huvuruga mfumo wa homoni na ukuaji wa mwili, huku ukiharibu mfumo wa urekebishwaji wa kiwango cha sukari mwilini unaoweza kumsababishia muhusika ugonjwa wa kisukari.
Jarida la Food and Fitness Advisor la Marekani limebainisha kuwa ni vyema baada ya kumaliza mazoezi kula vyakula vyenye kiwango kidogo cha wanga ambavyo huepusha magonjwa ya kisukari (aina ya pili) na magonjwa ya moyo.
Kwa hapa nyumbani mfano wa vyakula vyenye wanga kwa kiwango kikubwa ni viazi, mkate mweupe na muhogo.
Wataalamu hao wamesema kuwa mbali na vyakula vyenye sukari, ni vyema pia kujiepusha kunywa juisi au vinywaji vingine baridi vyenye sukari ya viwandani kwa sababu ya kujiepusha navyo ni kuepuka kubadili mpangilio mzima wa mwili.
Ushauri huu ni mzuri kuzingatiwa na wale ambao wanafanya mazoezi kwa lengo la kupunguza mwili kwani watakuwa wamefanikiwa kupunguza mafuta huku ukiwahusu pia wanaofanya mazoezi ya kurekebisha mwili kufikia malengo yao kwa kutobadili mfumo wa mwili.
Muhimu kwa kila anayefanya mazoezi mara baada ya kumaliza ni kunywa maji mengi ili kurudisha yale yaliyotoka kwa njia ya jasho.
Source: Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment