HII NI MAALUM KWAKO WEWE AMBAYE UNAPENDA KUIFAHAMU HIFADHI YA TAIFA YA WANYAMA YA SAADANI


Twiga ni miongoni mwa wanyama wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa Saadani
Asante kwa kuendelea kufuaatilia habarimkusanyiko.blogspot.com, na kama ilivyo kawaida yetu kila wiki siku ya Ijumaa huwa tunakuletea “JICHO LETU  PORI” na leo limeangukia kwenye vivutio vya asili vinavyopatikana hapa nchini Tanzania.

Tanzania imekuwa ni chaguo kubwa la wageni (Watalii) kutoka sehemu mbalimbali dunia, kwa lengo la kuja kuona na kujifunza katika vivutio vipatikanavyo Tanzania. Miongoni mwa baadhi ya vivutio hivyo ni pamoja na Mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu barani Afrika, fukwe nzuri za bahari ya Hindi pamoja na hifadhi kumi na sita zenye vivutio tofautitofauti.

Lakini leo “JICHO LETU PORINI” tutaangazia Hifadhi ya Taifa Saadani ( Eneo pekee ambalo nyika na bahari hukutana)

Hifadhi hii ya Saadani ni hifadhi namba kumi nchini na ina kilomita za mraba zipatazo 1100 na ilianzishwa mnamo mwaka 1995 na kuwa pori la akiba, lakini ilipitishwa rasmi kuwa hifadhi mnamo mwaka 2005.

Hifadhi hii imebeba jina la kijiji cha Saadani ambacho ni cha kihistoria kilichoanza kama kambi ya uvuvi katika karne 19. Jina la Saadani limetokana na kukosewa kutamkwa kwa maneno ya kiswahili ambayo ni ‘Saa’ na ‘ndani’. Maneno hayo yalikuwa yakitamkwa na mfanyabiashara wa kiarabu ambaye alikuwa anawaelekeza watu waliohitaji kujua muda (wakati) kipindi hicho wao walikuwa hawamiliki saa. Hivyo ilimbidi mfanyabiashara huyo kuwaelekeza saa iko ndani kwa kutamka saa-dani iliwaingie kuangalia wenyewe. Kutokana na suala hilo baadaye mfanyabiashara huyo alipewa jina la saa-dani ambalo alilikosea kutamka akiwa na nia yakusema saa iko ndani. Hapo ndipo mtaa alioishi mfanyabiashara huyo uliitwa saa-dani na ukawa ndio mwisho wa jina la Utondwe ambalo ndio lilikuwa jina la kijiji hicho kabla ya kuitwa Saadani.

MAHALI HIFADHI YA TAIFA YA SAADANI  ILIPO

Hifadhi ya Taifa Saadani ipo kando kando ya Pwani ya bahari ya Hindi katika mikoa ya Tanga na Pwani ndani ya wilaya za Bagamoyo, Pangani na Handeni. hifadhi hii ipo kaskazini mwa miji ya Dar es Salaam na Bagamoyo umbali wa kilometa 220km kwa kupita Chalinze-Msata-Mandera-Miono

VIVUTIO VYA UTALII VINAVYOPATIKANA HIFADHI YA TAIFA YA SAADANI
Fukwe nzuri zenye uasili wake

Aina mbalimbali za wanyama; Tembo, Simba, Nyati, Twiga, Pundamilia n.k

Zaidi ya aina 200 za ndege wakiwemo wale wanaohama (Heroe)

Mazalia ya kasa wa kijani

Maeneo mazuri ya mabaki ya kihistoria

Mila na desturi za wenyeji wa Pwani

SHUGHULI ZA UTALII

Kufanya safari za mtumbwi

Kuona vivutio vya utalii kwa gari

Kutembea kwa miguu hifadhini

Kubarizi ufukweni

Kuangalia ndege wa aina mbalimbali

Utalii wa usiku

JINSI YA KUFIKA HIFADHINI

Hifadhi ya Saadani hufikika kwa njia ya usafiri wa barabara, usafiri wa anga (ndege), usafiri wa reli (treni) na hata usafiri wa majini pia.

Ni vyema ukazingatia kufuata sheri za hifadhi kila unapokuwa ndani ya hifadhi. 

Jicho Letu Porini huandaliwa na Shadrack D. Daniel muongozaji wa watalii kutoka Kampuni ya Sam’s Car Rental Tour & Safar’s Ltd, hivyo tunakusihi kuungana nasi ili ufahamu zaidi kuhusu maisha ya wanyama pamoja na vivutio vyetu vya hapa nchini Tanzania

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname