MADUKA YA DAWA KUANZISHWA MAENEO YOTE NCHINI




 Bohari ya Dawa nchini (MSD) imesema inatarajia kuanzisha maduka ya dawa katika maeneo yote ya nchi kwa lengo la kurahisisha usambazaji wa dawa na vifaa tiba.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Cosmas Mwaifani alisema mpango huo utakaosimamiwa na ofisi zao za kanda ni sehemu ya mkakati wa kujipanga katika misingi ya kujiendesha kibiashara.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa pili wa miaka sita unaoanzia 2014 hadi 2020 kwa ajili ya kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa urahisi nchi nzima hadi ngazi ya vituo vya afya.

“Ifikapo Januari 30, 2015 bohari itatekeleza mabadiliko makubwa yenye lengo la kuhakikisha dhima ya kuwezesha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora kwa bei nafuu kwa Watanzania wote inatekelezwa kwa vitendo,” alisema Mwaifani

Mwaifani alisema maduka hayo yatafanya kazi saa 24 na kuuza dawa kwa bei nafuu iliyo chini ya bei ya soko na yatatoa huduma kwa watu binafsi na waliopo chini ya utaratibu wa Bima za Afya watakaokuwa wameandikiwa vyeti vya dawa na vifaa tiba.

Aidha, Mwaifani alifafanua kwamba maduka hayo yatatoa huduma hizo kwa hospitali zote za binafsi na za Umma pamoja na maduka yote ya dawa yatakayohitaji kununua dawa kwa bei ya jumla.

Mwaifani aliendelea kusema kuwa hatua hiyo itaongeza wigo wa bohari kusambaza dawa na kuiondoa katika mfumo wa sasa wa kutoa dawa kwa mahitaji maalum, hivyo kuboresha huduma za afya zinazotolewa katika hospitali na vituo vya afya vilivyosajiliwa kutoa huduma za afya na kuipunguzia Serikali mzigo wa kuchoma dawa zilizopita muda wake.

Katika hatua nyingine, alisema MSD inatarajia kuanzisha utaratibu wa kutumia wazalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba ili kuepuka gharama ya zaidi ya Dola100 milioni za Marekani inazotumia kwa mwaka kuagiza asilimia 85 ya dawa na vifaa hivyo nje ya nchi. Huku akisema kuwa kutokana na hali hiyo kiwango cha upatikanaji wa dawa nchini kimekuwa chini ya asilimia 85 na kuigharimu fedha nyingi kutunza dawa kwa muda mrefu kutokana na kufidia muda mrefu wa miezi tisa ya tahadhari kufidia muda mrefu unaotumika kuanzia manunuzi hadi kufikisha dawa hizo nchini.

Amesema zipo dawa na vifaa tiba ambavyo vinaweza kuzalishwa hapa nchini kwa gharama ndogo au kutumia malighafi zipatikanazo hapa hapa hivyo mchakato wa kuwapata washirika katika mradi huo utafanyika kupitia mzabuni atakayetangazwa rasmi.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname