MGOMBEA URAIS MWAKANI ATABIRIWA KIFO
Mtabiri maarufu nchini Maalim Hassan Hussein, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mtabiri maarufu marehemu Sheikh Yahya Hussein, ametabiri mambo yatakayotokea mwakani (2015), likiwamo tukio la kufariki ghafla kwa kiongozi mmoja ambaye ni mzee na yumo kwenye mbio za kutaka kuwania urais mwakani.
Hussein alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo kuwa kiongozi huyo atadondoka ghafla kwenye jukwaa na kufariki dunia wakati akipelekwa hospitali.
“Kiongozi huyo atakufa wakati akipelekwa hospitalin,” alisema Hussein
Mbali na kutabiri kifo hicho, pia Hussein alisema mwandishi mmoja mashuhuri hapa nchini atakufa kifo chenye utata kitakachoitesa Serikali na familia yake katika kutafuta sababu za kifo chake. Huku akiongeza kwamba nyota inaonesha kwamba misiba miwili ya kitaifa itatokea mwakani.
Aidha, kuhusu uchaguzi wa kiti cha urais mwaka 2015, alisema kati ya kundi la vijana na wazee, nyota zinaonesha kwamba watakaofaidika ni vijana.
“Lakini kuna wazee pia wanaoweza kufaidika, hawa ni wale wenye sura za ujana, yaani babyface au wenye kupenda mambo ya ujana na kushirikiana na vijana,” alisema.
Pia aliongeza kuwa ili Tanzania ilinde sifa ya kuwa nchi yenye amani na utulivu ni kuwa na Rais kijana mwenye mchanganyiko wa dini mbili au mwenye ndoa ya dini tofauti.
Pamoja na hayo, alisema utabiri unaonesha kuwa mwaka 2015 utatawaliwa na nyota yenye kupendelea vijana, hivyo ni vyema vyama vya siasa vikawasimamisha kugombea nafasi za urais, ubunge na udiwani, huku akibainisha kuwa mauaji, fujo na ghasia vitatawala katika uchaguzi ujao na kwamba Serikali inatakiwa kuweka tahadhari kubwa.
Hata hivyo, Hussein alienda mbali zaidi na kutabiri kuwa viongozi wawili wa siasa na dini kukumbwa na kashfa ya ngono itakayowasababisha anguko la utumishi wa kutukuka na familia zao.
Mbali na hayo, alisema mwaka ujao utakuwa na mafuriko na dhoruba vitakavyosababisha madhara, hivyo tahadhari ni vyema ichukuliwe kuanzia sasa.
Halikadhalika aliendelea kusema kuwa kutakuwa na vifo vya ghafla vya wasanii, wanamichezo na watu maarufu kama ilivyokuwa kwa mwaka 2014.
Sambamba na hayo Maalim Hussein alisema lile tishio la wahisani kuiwekea Tanzania vikwazo vya kiuchumi, litalegezwa na kuifanya nchi kuingia katika Uchaguzi Mkuu kwa staha. Huku akiongeza kwa kusema kuwa wazee wataendelea kushutumiana na kupingana hadharani, hali itakayosababisha migawanyiko ndani ya vyama vya siasa na nchi kwa jumla.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment