Baada ya kuwepo kwa mashinikizo kutoka kwa watu wa kada mbalimbali hapa nchini juu ya kumtaka Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuachia ngazi kufuatia kuhusishwa na sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, hatimaye waziri huyo ametangaza kujiuzulu wadhifa wake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Profesa Muhongo amesema kwamba anaamini kujiuzuru kwake kutaisaidia serikali na Bunge kutuliza malumbano juu ya sakata hilo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo.
Hata hivyo, Profesa Muhongo pamoja na uamuzi wake huo amesisitiza kwamba yeye si mwizi na hawezi kuuza utu wake kwa kupewa rushwa ili kuwakandamiza wananchi.
Profesa Muhongo alisema “nimeamua kujiuzuru kwa dhati kabisa bila kushinikizwa na mtu yeyote, inaonekana mimi ndiyo nitamaliza mjadala huu wa sakata la Escrow”
Profesa Sospeter Muhongo akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam wakati aktangaza uamuzi wake wa kujiuzuru. |
Aidha, Profesa Muhongo alisema kuwa kuna mambo mengi ya kitaifa yanayotakiwa kujadiliwa, lakini watu wamekazana na Escrow .
Mbali na hayo, Profesa Muhongo amesema kuwa pamoja na kujiuzuru anatarajia mapema kuzungumza na Watanzania ili kuwaeleza ukweli wa sakata la Escrow na kujiuzuru kwake ili kuvunja majungu yanayoendelea kuitesa Tanzania na watu wake.
Hali kadhalika, amesema kuwa amelelewa katika malezi yenye maadili mema na kwamba tokea alipomaliza masomo yake aliaswa kutopokea ama kutotoa rushwa, hivyo hawezi akapokea rushwa kwa ajili ya kuutukana utu wa mtanzania hicho ndicho kinachomgharimu.
Sambamba na hayo, Profesa Muhongo ameelezea furaha yake ya kupatikana kwa maendeleo ya haraka katika wizara yake kwa kipindi chake, huku akisema kuwa nidhamu na uwajibikaji vilikuwa dira ya maendeleo wizarani hapo.
No comments:
Post a Comment