Mwanajeshi wa kikosi cha anga cha
Indonesia akiwa kwenye helikopta ya kutafuta miili na mabaki ya ndege ya
AirAsia.
|
Mkuu wa shirika la msako na uokozi la Indonesia Fransiskus Bambang Soelistyo amewaambia waandishi wa habari mjini Jakarta kwamba wamegunduwa vipande vinne vikubwa vya mabaki ya ndege hiyo ambavyo wamekuwa wakiitafuta.
Ugunduzi huo umefuatiwa wakati serikali ikisema kwamba shirika la ndege la AirAsia limekiuka masharti ya leseni yake ya kutumia njia ya Surabaya kwenda Singapore hapo Jumapili siku ambayo ndege yake hiyo aina ya Airbus A320-200 ilipoanguka kwenye bahari ya Java na kutangaza kwamba watachunguza ratiba nyingine za safari ya ndege za shirika hilo.
Ndege ya shirika la ndege la AirAsia chapa Airbus 320-200 mfano wa ile iliyopata ajali |
Mbali na hayo afisa mwingine wa timu hiyo ya uokozi Supriyadi ambaye anaratibu operesheni za uokozi kutoka bandari ya Pangkalan Bun ilioko Borneo amesema hapo awali kwamba hali ya kutoweza kuona vizuri imekwamisha juhudi za kunasa taswira za vipande hivyo kwa kutumia vyombo vya kuzamia chini ya bahari.
Hadi sasa hakuna manusura waliogundulika kutokana na ajali hiyo ambayo ilitokea kama dakika 40 baada ya ndege hiyo kuruka kutoka Surabaya mji wa pili kwa ukubwa nchini Indonesia katika eneo ambalo linafahamika kwa kuwa na vimbunga vikali hususan wakati huu wa msimu wa mvua.
Sambamba na hayo ripoti kutoka katika ofisi ya utabiri wa hali ya hewa nchini Indonesia imesema yumkini ndege hiyo imeruka kwenye hali mbaya ya hewa jambo ambalo ingelikuwa vigumu kuliepuka na kwamba inawezekana hali hiyo imesababisha kuganda kwa barafu kwenye engine za ndege hiyo.
Ofisi hiyo imesema kwa kuzingatia data zilizopatikana mara ya mwisho juu ya mahala iliokuweko ndege hiyo hali ya hewa imesababisha ajali hiyo.
Wakati hayo yakiendelea Djoko Murdjatmondo ambaye ni kaimu mkurugenzi mkuu wa Usafiri wa Anga nchini Indonesia amesema hapo Jumamosi kwamba Wizara ya Uchukuzi itachunguza njia nyingine za safari zinazotumiwa na ndege za shirika hilo ambayo husafiri katika vituo 15 nchini Indonesia. Huku akiongeza kwamba watachunguza ratiba za safari zote za ndege za shirika hilo la AirAsia na kwamba wanataraji kuanza kufanya hivyo hapo Jumatatu, lakini kumekuwa na uwezekano wa leseni ya shirika hilo la AirAsia nchini Indonesia ikafutwa.
No comments:
Post a Comment