TBS YATEKETEZA CHUMVI ILIYOTENGENEZWA CHINI YA KIWANGO


Kiasi cha tani 1.5 cha chumvi yenye thamani ya shilingi 500,000 kutoka kampuni ya Seasalt kimeteketezwa baada ya kugundulika kutokidhi viwango.


Uteketezaji wa chumvi hiyo umesimamiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kufuatia agizo la Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda la kuondolewa sokoni bidhaa hiyo na kufungwa kwa kiwanda hicho mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuteketeza bidhaa hiyo, Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile, alisema wamechukuwa hatua ya kuiondoa bidhaa hiyo sokoni kama ilivyoagizwa na waziri Kigoda.

‘’Baada ya uchunguzi na maabara imebainika kwamba chumvi hiyo haina madini joto badala ya kuwa na milligram 30 mpaka 60 kwa kilogramu moja, lakini imekuwa na milligram 12 ambayo ilikuwa ni chini kwa matumizi ya binadamu” alisema

Aidha, alitoa wito kwa watanzania wanaposikia tangazo lolote kutoka TBS kuhusu bidhaa ambazo zipo chini ya kiwango wasiendelee kununua na kuzitumia.

Naye meneja masoko wa kampuni ya Seasalt Rajesh Verma alikiri bidhaa hiyo kuwa chini ya kiwango na kuwa wao wanajali afya ya mtumiaji na ndio maana wametekeleza agizo lililotolewa.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname