WAZAZI WAASWA KUACHA KUWAJENGEA WATOTO MITAZAMO YA KUAJIRIWA


WAZAZI nchini wametakiwa kuwapeleka watoto shule na kuwajengea uwezo katika kujiajiri kuliko kutegemea kuajiriwa serikalini.

Akizungumza na mwandishi wa blog hii ofisini, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kutengeneza Ajira Tanzania (Tahec), Samwel Magoiga, alisema umefika wakati wa kuleta mabadiliko katika soko la ajira nchini.

“Vijana wengi wanasoma wakiwa na lengo la kutaka kuajiriwa serikalini, wakati uwezo mkubwa wa kujiajiri na kubadilisha soko
la ajira nchini upo” alisema Magoiga.

Pia amesema kuwa, taasisi yake imekuwa mstari wa mbele katika kuwajengea uwezo wahitimu wa shule ili waweze kuongeza ushindani katika soko la ajira, licha ya kuwapo kwa changamoto ya utozaji kodi.

“Tatizo kubwa ni mifumo ya kodi zetu ambayo siyo rafiki kwa wajasiriamali wanaoanza, kungekuwa na kibali angalau kwa wanaoanza wawe na punguzo la kodi kwa walau miaka mitano ya kwanza,” alisema.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2011 na hadi sasa imefanikiwa kuwafanikisha vijana 35 kuingia kazini, ambao wameajiriwa na kutoa mafunzo kwa vikundi 20 vya kijasiriamali.

Magoiga alisema yeye na wenzake kadhaa waliamua kuanzisha taasisi hiyo baada ya kubaini kuwa wahitimu wengi wa elimu ya sekondari na vyuo mbalimbali huishia kukosa ajira nchini.

Pamoja na hayo, aliwataja waasisi wenza wa taasisi hiyo kuwa ni Melkiades Kibirigi, ambaye kwa sasa ndiye Mhasibu, Raphael Kibirigi (Katibu), Daliva Barugize (Mkurugenzi Msaidizi), Yusuf Paulo (Mwanachama) na Jacob John (Mshauri Elekezi).

Habari hii imeandaliwa na Goodluck Ngowi ambaye ni mwandishi wa blog hii kwa upande wa jijini Mwanza. Asante kwa kuendelea kuwa nasi msomaji wetu. 

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname