Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) limetakiwa kujiendesha kibiashara na kufanya shughuli zake kwa kuzingatia maadili ili liwe shirika linalofanya kazi vizuri na kutimiza wajibu wake.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati alipokutana na Bodi ya Wakurugenzi ya TBC, Dar es Salaam jana.
Nape alikutana na bodi hiyo katika utaratibu wa kawaida wa kukutana pamoja na kuzungumzia masuala mbalimbali ya shirika hilo lililo chini ya wizara hiyo.
“Tumeamua mambo kadhaa ya kuisaidia TBC ijiendeshe kibiashara na hili ni kubwa kwa kuangalia maeneo ya uwekezaji na namna ya kuongeza vyanzo vya mapato na kubana matumizi ambayo si ya lazima yakiwepo ya bodi yenyewe kuangalia baadhi ya vitu,” alisema Nape.
Akizungumzia suala la hamasa ya utendaji kazi ya wafanyakazi wa shirika hilo, Nape alisema kabla hawajaingia huko kwa watumishi wameona ni vyema kwanza wao wakaangalia yale mambo muhimu ambayo ndiyo yatafanya kuleta hamasa kwa wafanyakazi.
“Tumezungumza mambo mengi ikiwemo ufanyaji kazi wa bodi, mambo ya watumishi hasa na kikubwa ni suala la morali ya kazi ya wafanyakazi wa TBC, maslahi yao, jinsi wanavyofanya kazi, vitendea kazi na mambo mengine ya msingi ambayo yanahakikisha shirika hili linakuwa moja ya mashirika yanayofanya kazi vizuri na kutimiza wajibu wake,” alisema Nape.
Nape alisema yapo mambo ambayo wamekubaliana na bodi na kushauriana kwa pamoja na katika utekelezaji patarajiwe mabadiliko makubwa huku akisema kuna hatua kadhaa walizokubaliana na bodi hiyo kufanyika.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TBC, Profesa Mwajabu Possi alisema wamepokea maelekezo ya waziri na wameahidi kuyafanyia kazi huku akisema na wao kuwa wamemweleza changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili katika uendeshaji wa shirika hilo.
CHANZO: mtembezi.com
No comments:
Post a Comment