WAZAZI WALALAMIKIA GHARAMA ZA UANDIKISHAJI WATOTO SHULE



Ikiwa ni siku chache tangu shule kufunguliwa nchini, baadhi ya wazazi wanao wapeleka watoto wao kuanza elimu ya msingi katika shule ya msingi Mwenge, kata ya Nyamanoro wilayani lIemela jijini Mwanza, wamelalamikia uongozi kuwatoza gharama kubwa za uandikishaji kinyume na utaratibu wa serikali.



Mmoja wa wazazi ambaye hakupenda jina lake liandikwe mtandaoni, alisema kuwa alimpeleka mwanaye kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo na akatakiwa kulipia gharama ya shilingi 90,000 pamoja na shilingi 2000 kwa ajili ya madaftari.

‘’ Nashangaa nimempeleka mtoto kuanza elimu ya msingi, ajabu nikaambiwa nilipie shilingi 90000 kwa ajili ya uandikishaji pamoja na shilingi 2000 kwa ajili ya madaftari, jambo ambalo ni geni kwangu na sijajua utaratibu huo umetoka wapi na umeanza lini?”
alihoji mzazi huyo.

Aidha, mzazi huyo alisema anachofahamu mwongozo na sera ya elimu, inatolewa bure na hivi karibuni serikali imetangaza kufutwa kwa michango yote inayohusu elimu kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.

Naye Mkuu wa shule hiyo, Alex Mapesa, akifafanua kuhusu uchangiaji wa gharama hizo, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa, wazazi wanatakiwa kulipa shilingi 90000, mtoto anapoanza shule, hiyo ianfuatiwa baada ya kukubaliana kwenye kikao cha wazazi na kamati ya shule cha Novemba 25 mwaka jana .

Alisema shilingi 54,000 ni kwa ajili ya sare za shule ambazo ni sweta, shati, fulana, tai, lebo, soksi na sare ya michezo kwa wavulana watapatiwa kaptura pamoja na kaushi (singlendi) ya kuvalia ndani, ambapo wasichana watapata sketi na shumizi (spice),vinavyo patikana shuleni hapo japo si lazima kwa mzazi kununua hapo,ni uamuzi wake yeye ila anatakiwa kumpatia mtoto sare zinazoendana na wenzake.

Hata hivyo, Mapesa alisema shilingi 36000 ukijumlisha ndiyo unapata gharama ya shilingi 90000, zinatolewa kwa ajili ya ukarabati wa shule, ikiwemo kurekebisha madarasa kwa kuweka vigae, kupaka rangi, kulipa watumishi wanaofanya usafi wa mazingira ikiwemo uwanja, bustani, vyoo, madarasa, taaluma, kulipa ankara ya umeme na maji.

Mbali na fedha hizo alisema pia sh2000 ni kwa ajili ya madaftari na kalamu atakayopewa mwanafunzi kwa mwaka mzima bila kulipia tena, lakini mzazi halazimishwi bali ni uamuzi wake kuchangia fedha hiyo au amnunulia pindi daftari linapohitajika.

Sambamba na hayo alisisitiza kuwa makubaliano hayo ni ya kamati ya shule na wazazi, hivyo ni wajibu wake kusimamia na kutekeleza, na hayupo tayari kuona shule yake ikiwa katika muonekano ambao siyo mzuri na ukizingatia ipo jirani na soko la kimataifa linalotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni litakalokuwa na watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Pia Mapesa aliwaomba wazazi na jamii kujitoa katika kuchangia michango ya shule ili kuwatengenezea mazingira mazuri ya watoto kusoma na kufanya vizuri, kwani tokea waanze mpango huo wazazi wengi wanawapeleka watoto wao hapo kwani mpaka sasa wameisha pata wanafunzi 114 wanaoanza elimu ya msingi, jambo ambalo ni tofauti na shule zingine.
Habari hii imeandaliwa na kuandikwa na Goodluck Ngowi, ambaye ni mwakilishi wa habarimkusanyiko.blogspot.com kutoka jijini Mwanza, tafadhali endelea kuwa nasi msomaji wetu kwa lengo la kupata habari zaidi.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname