EBOLA BADO NI TATIZO MAGHARIBI MWA AFRIKA


Mkuu wa masuala ya kupambana na Ebola wa Umoja wa Mataifa Daktari David Nabarro, amesema itachukua miezi kadhaa zaidi kabla ya janga la Ebola kuweza kudhibitiwa katika nchi za magharibi mwa Afrika zilizoathirika.

Daktari Nabarro amebainisha kuwa kuna mabadiliko makubwa ya hali ilivyo katika nchi zilizoathiriwa na Ebola magharibi mwa Afrika katika kipindi cha miezi minne iliyopita kutokana na jinsi serikali husika zinavyoushughulikia ugonjwa huo,hatua zinazochukuliwa na jamii na mchango wa jumuiya ya Kimataifa katika kupamabana nao.

Hata hivyo, amesema juhudi zaidi zinahitajika kuudhibiti ugonjwa huo magharibi mwa Sierra Leone na kaskazini mwa Mali ili kupunguza idadi ya visa vipya Liberia na kupunguza maambukizi Mali.

Nalo Shirika la afya duniani WHO limekiri kuwa halikuweza kufikia lengo la kuwatenga wagonjwa wote wa Ebola na kuwazika salama waliokufa katika taifa la Sierra Leone kwa asilimia 70 ilipofika tarehe mosi mwezi huu kama ilivyokuwa imetarajia.

Mbali na hayo WHO imesema kuwa inakuwa ni vigumu kwao kusawazisha takwimu kuhusu visa vya Ebola kwa sababu haijui hasa ni wagonjwa wangapi waliogua Ebola na kuwafuatilia walio karibu nao inakuwa kibarua kigumu.

Huku hayo yakijri, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon hapo jana alimtangaza Ismail Ould Cheikh Ahmed kuwa mkuu mpya wa operesheni za kupambana na Ebola magharibi mwa Afrika ambapo hapo awali wadhifa huo uliokuwa ukishikiliwa na Anthony Banbury.

Ahmed ambaye hivi sasa ni Naibu wa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya atafanya kazi kwa karibu na Nabarro na serikali za kanda hiyo ya magharibi mwa Afrika kuanzia mwezi Januari atakapochukua rasmi wadhifa huo.

Itakumbukwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon mwezi uliopita alisema janga hilo la Ebola huenda likadhibitiwa baadaye mwaka ujao. Huku kiasi cha watu 18,100 wameathirika na 6,500 kati yao wamefariki nchini Guinea,Liberia na Sierra Leone.



Asante kwa kuendelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com tunathamini sana uwepo wako msomaji wetu


No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname