WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA WAAPISHWA, HUKU BAADHI YAO WAKITUHUMIWA KUTOSHINDA KIHALALI



WENYEVITI na wajumbe walioshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Disemba 14 mwaka jana, kutoka kata nne zilizopo wilayani Ilemela jijini Mwanza wameombwa kufanya kazi kwa uadilifu na
kuwatumikia wananchi kwa moyo, bila kujali itikadi za vyama, dini wala ukabila.

Wito huo umetolewa na mtendaji wa kata ya Kirumba Abdulaham Kamapa, wakati wa zoezi la uapishwaji wa wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa, kutoka kata ya Kirumba, Ibungilo, Kitangiri na
Nyamanoro, iliyofanyika shule ya msingi Kitangiri mbele ya Afisa uchaguzi wa wilaya ya Ilemela na mwanasheria Goodluck Lukandiza.

“Uongozi ni moyo inayoendana na kufanya kazi kwa uadilifu, hivyo ni wajibu wenu kufanya kazi kwa haki bila upendeleo wala kujali itikadi za kidini, kabila, kwani mpo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi
na siyo kujinufaisha wewe na chama , hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye enda kinyume na maadili ya kazi” alisema Kapama

Naye Salum Salumu ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkudi kupitia Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) alisema zoezi la uapishwa limeenda vizuri ila zimetokea changamoto ndogo ndogo ikiwemo kufanyiwa vurugu kwa baadhi ya wenyeviti ambao wanatuhumiwa na wenzao kuwa hawakushinda kihalali na badala yake wametumia nguvu, ambao ni kutoka katika kata nne ikiwemo
Kitangiri, Nyamanoro, Kirumba na Ibungilo na kuja kuapishwa wakiwa wamesindikizwa na Polisi.

Salum aliendelea kusema kwamba kutokana na kitendo hicho anaona kuwa Serikali haijawatendea wananchi haki na kupuuza kura zao kwa kuwaweka viongozi wanaowataka na kuwaacha walochaguliwa na wananchi,jambo ambalo wanawaachia wananchi waweze kutoa hukumu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kitangiri kati kupitia Chama cha Mapinduzi
(CCM) Saidi Hamis, ambaye ni mmoja wa viongozi wanaotuhumiwa kuapishwa wakati hajashinda alisema kuwa alishinda katika uchaguzi huo kwa kuchaguliwa na wananchi, hivyo kuwaomba wale wote wanaodai kuwa hakushinda waende kufungua kesi mahakamani na sheria zifuate kuliko kufanya fujo na kuvunja amani ya nchi na kwa jamii.

Saidi Hamis pia aliiomba serikali kuangalia jambo la vurugu kwa umakini zinazoendelea kutokea hasa katika kipindi cha uchaguzi na kuzidhibiti, ili kuepuka madhara makubwa katika uchaguzi mkuu, huku akisema kwamba anaamini bila kudhibiti jambo hili amani tunayojivunia itatoweka.

Pamoja na hayo, kuendelea Afisa Uchaguzi wa wilaya ya Ilemela na Mwanasheria Goodluck Lukandiza, alisema zoezi la uapishwaji wa wenyeviti na wajumbe kutoka katika kata hizo limeenda vizuri japo kulikuwapo na changamoto ya wenyeviti wachache kutoapishwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ugonjwa, safari na kufanyiwa fujo, hivyo watapanga siku nyingine ndani ya wiki hii na kisha kuwaapisha.

Pia Lukandiza aliwataka wale walioapishwa kutende kazi zao sawasawa na sheria inavyoelekeza, huku akiongeza kuwa waliofanya fujo wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwani sehemu ya kuapisha hapakuwa mahala sahihi pakuleta malalamiko, na kuwataka waende mahakamani kufungua kesi ya kutoridhika na ushindi wa kiongozi husika.
Habari hii imeandaliwa na Goodluck Ngowi, ambaye ni mwakilishi wa habarimkusanyiko blog kutoka jijini Mwanza, tafadhali endelea kuwa nasi tukupatie habari za kila kona ya Tanzania Rafiki.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname