HATIMAYE RAIS UHURU KENYATTA AMESAINI SHERIA YA USALAMA





Rais Uhuru Kenyatta
Baada ya kuwapo kwa vuta nikuvute hapo jana katika Bunge la nchini Kenya, hatimaye Rais Uhuru Kenyatta, amesaini na kuiidhinisha sheria mpya ya usalama ambayo inawezesha majasusi kunasa mawasiliano kisiri au kufanya udukuzi pamoja na kuwazuia washukiwa wa ugaidi kwa mwaka mmoja kabla ya kuwafungulia mashitaka.

Akisaini sheria hiyo mpya Kenyatta amesema kuwa sheria hiyo haikiuki haki za binadamu wala kuwapokonya watu uhuru wa kujieleza, huku akiongeza kuwa sheria hiyo mpya ni muhimu nchini Kenya kwa sasa kwani inahitajika kwa ajili ya kukabiliana na tisho la ugaidi kutoka kwa kundi la wapiganaji wa kiislamu la Al Shabaab.

Mnamo siku ya Disemba 17 siku ya Alhamis wabunge wa serikali na wale wa upinzani walipigana na kurushiana maneno makali bungeni wakijadili marekebisho kwenye mswaada huo kabla ya Rais kuupitisha kuwa sheria, ambapo katika vurugu hizo mmoja wa wabunge wa upinzani alimmwagia maji naibu spika.

Aidha, sheria hizo mpya zilipitishwa na bunge licha ya pingamizi kubwa na vurugu kutoka kwa wabunge hao wa upinzani.

Wakati hayo yakijili vyombo vya habari nchini humo pia vimepiga kelele vikieleza kuwa baadhi ya vipengee vya sheria hiyo vinabana uhuru wa vyombo vya habari na hata kutishia kwenda mahakamani.

Mswada huo kabla ya kutiwa saini na kufanywa sheria,ulifanyiwa mabadiliko kadhaa katika vipengee ambavyo vilionekana na baadhi ya wabunge kama vilivyokua vikali na kwenda kinyume na katiba.

Polisi sasa watakuwa na jukumu la kuidhinisha taarifa au picha za uchunguzi wa maswala ya usalama na hasa kuhusiana na ugaidi.

Polisi pia ndio watapaswa kuidhinisha picha za waathiriwa wa ugaidi kabla ya kuchapishwa au kuoneshwa katika vyombo vya habari.

Vyombo vya habari vinasema haya yanakwenda kinyume na uhuru wa vyombo vya habari Adhabu itakayotolewa kwa watakaokiuka sheria hii ni hadi faini ya shilingi milioni tano au dola elfu sitini ama kufungwa jela kwa zaidi ya miaka mitatu.

Asante sana kwa kufanya maamuzi ya kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname