JAMII IMETAKIWA KUWASAIDIA NA KUWAPENDA WATU WENYE ULEMAVU



Kumekuwepo na tabia ya baadhi ya watu kutenga na hata kuwaficha watoto wenye ulemavu, kufuatia tabia hiyo wito umetolewa kwa jamii na kuitaka kuachana na tabia hiyo, badala yake iwasaidie misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye vituo vinavyotoa huduma hizo endapo wanapoona kushindwa kuwatunza.

Akizungumza Ofisini kwake, Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu jijini Mwanza (CHAWATA), Bw; Vicent Ludomya, alisema wadau pamoja na viongozi wa dini na serikali kuanzia ngazi ya
vijiji wanapaswa kuwasaidia walemavu wa ngozi na kujua matatizo yanayowakabili.

“Tunaamini jamii bado ina watu wa namna hii wenye tabia ya kuwatenga walemavu, wao pia wana haki ya kuishi na kufurahi kama binadamu wengine” alisema Ludomya

Aidha, Ludomya alisema kwamba kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na kikundi cha madaktari kutoka nje ya nchi kwa kushirikiana na Chawata Taifa ulibainisha kuwa kaya masikini ndio zinahistoria za kuwa na watu wenye ulemavu zaidi hii ni kutokana na kuwa kaya maskini zipo hatarini kujifungua watoto wenye ulemavu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utindio wa ubongo, matege, ulemavu wa akili kutokana na hali ya uchumi kuwa mbaya na hivyo kushindwa kuwapeleka kina mama hospitalini mapema pale wanapohitaji matibabu.

Mbali na hayo, Ludomy alizitaja sababu nyingine zinazopelekea kuwepo kwa watu wenye ulemavu ambazo ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya kwa wazazi, uvutaji wa sigara, magonjwa ya kurithi pamoja na kuugua maradhi kama kisonono na kaswende sambamba na mama mjamzito kuugua malaria kali na kushindwa kuitiba kwa muda mwafaka.

Hapo awali Bw: Ludomya alisema takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 216 chini ya umri wa miaka 18 kutoka sehemu tofauti mkoani mwanza kuanzia mwaka 2009 hadi 2014, waliripotiwa kwenye kituo cha walemavu, huku jumla ya wanawake 51 wakiripotiwa kuachwa na waume zao kwa sababu ya kujifungua watoto wenye ulemavu.

Story hii imeandaliwa na Goodluck Ngowi mwakilishi wa habarimkusanyiko.blogspot.com kwa mkoa wa Mwanza.

Ni haki yako kuzipata habari zote zinazojili kila wakati kutoka hapa nchini na nje pia, tafadhali endelea kuwa nasi

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname