WABUNGE WARUSHIANA NGUMI BUNGENI


Wabunge wa Kenya wametofautiana vikali bungeni na kushikana mashati pamoja na kurushiana ngumi kufuatia mjadala kuhusu mswada tatanishi wa usalama ambao wabunge wa upinzani wanasema unakiuka uhuru wa wakenya.

Kufuatia kutofautiana huko bunge lililazimika kuahirisha vikao vyake kwa dakika 30 badala ya kujadili mswada tatanishi kuhusu usalama wa nchi. Kikao hicho kilikuwa ni kikao maalum ambacho kilipaswa kupitisha mswada huo ambao baadaye utaidhinishwa na Rais kuwa sheria.

Wabunge wa upinzani walipinga mswada huo na kuanza kurusha karatasi sakafuni huku wakikatiza shughuli bungeni humo.

Aidha, mwenyekiti wa kamati ya usalama wa bunge, Bwana Asman Kamama, alijaribu kuyajadili mabadiliko yaliyopendekezwa kufanyiwa mswada huo, lakini wabunge walianza kuimba na kumzomea spika wa bunge wakiukataa mswada huo wakisema 'bado mapambano.'

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Spika wa bunge Justin Muturi aliamuru walinzi wa bunge kuwaondoa baadhi ya viongozi waliofika bungeni humo kwa mjadala ambao ulitarajiwa kuwa kaa moto, hasa kwa upande wa upinzani.

Mswada huo ambao umewasilishwa bunge kufuatia matukio ya utovu wa usalama na mashambulizi nchini Kenya, unapendekeza kuwa washukiwa wa ugaidi wanaweza kuzuiliwa kwa mwaka mmoja huku polisi wakifanya uchunguzi.

Mapendekezo ya mswada huo ni kwamba mshukiwa wa ugaidi anaweza kuzuiliwa kwa siku 360 kutoka siku 90 za awali.

Pia ikiwa mswada huo utapistihwa kuwa sheria, mashirika ya habari yatatozwa faini ya hadi shilingi milioni 5 kwa kuchapisha taarifa au picha ambazo zinaleta hofu na kusababisha taharuki.

Mswada huu umetolewa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Al Shabaab wakilalamika na kutaka wanajeshi wa Kenya kuondolewa Somalia

Rais Kenyatta amekuwa akikabiliwa na shinikizo kuimarisha usalama tangu mashambulizi ya Septemba mwaka 2013 katika jengo la maduka ya kifahari la Westgate mjini Nairobi ambapo watu 67 waliuawa.

Endelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com kwa habari zaidi

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname