WAKURUGENZI WATENGULIWA KWA KUTOTIMIZA WAJIBU WAO UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA



Serikali imetengua uteuzi wa wakurugenzi sita wa Halmashauri mbalimbali hapa nchini walioshindwa Kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uchaguzi huo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh. Hawa Ghasia wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari  jijini Dar es Salaam uliolenga kutoa taarifa ya hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kwa wale wote walisababisha kasoro mbalimbali katika uchaguzi huo.

Akitaja majina ya Wakurugenzi ambao uteuzi wao umetenguliwa Mh. Ghasia amesema kuwa ni Bw. Benjamin A. Majoya ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuranga, Bw.Abdalla Ngodu Mkurugenzi Mtendaji Kaliua, Bw.Masalu Mayaya Mkurugenzi Mtendaji Kasulu, Bibi Goody Pamba Mkurugenzi Mtendaji Serengeti, Bw.Julius A. Madiga Mkurugenzi Mtendaji Sengerema na Bw. Simon C.R. Mayeye Mkurugenzi Mtendaji Bunda.

Aidha, akizungumzia wakurugenzi waliosimamishwa kazi Mh. Ghasia amesema ni watano na wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi zaidi wa kiwango cha ushiriki wao katika kasoro zilizojitokeza kwenye Halmashauri zao ambao ni Bw.Felix T. Mabula wa Hanang, Bw. Fortunatus Fwema wa Mbulu, Bibi Isabella D. Chilumba wa Ulanga,Bibi Pendo Malabeja wa kwimba na Bw. Wiliam Z. Shimwela wa Manispaa ya Sumbawanga.

Mbali na hao wakurugenzi waliopewa onyo kali na ambao watakuwa chini ya uangalizi kubaini kama wana udhaifu mwingine ili wachukuliwe hatua zaidi Mh. Ghasia amesema kuwa ni watatu, ambao ni Bw. Mohamed A. Maje wa Rombo, Bw. Hamis Yuna wa Busega, Bw. Jovin A. Jungu wa Muheza.

Pia Mh. Ghasia aliwataja wakurugenzi wengine watatu waliopewa onyo na kutakiwa kuongeza umakini wanapotekeleza majukumu yao ambao ni Bw. Isaya Mngulumi Manisapaa ya Ilala, Bw. Melchizedeck Humbe Humbe wa Hai na Bw. Wallace J. Karia wa Mvomero.

Pamoja na hayo Mh. Ghasia ametoa wito kwa watumishi wa Umma na Viongozi wa Sekta ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambapo amesema kwamba kila mmoja anao wajibu wa kutekeleza kwa weledi na uadilifu ili kuepuka kasoro zinazoweza kuepukwa.

Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI ilitimiza wajibu wake wa kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika kwa ukamilifu kwa kutoa miongozo na mafunzo kwa watendaji wa Halmashauri ambapo Mikoa na Halmashauri ziliwezeshwa kwa fedha ili kugharimia maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na kuandaa vifaa na karatasi za kupiga kura.
Asante kwa kuwa nasi tafadhali endelea kutuunga mkono daima, nasi tuanahidi kukupatia kila story tunayoipata


No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname