Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) Mkoa wa Mwanza, wameiomba Serikali kutowanyanyapaa, badala yake wawajali kwa kuwatimizia mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na elimu.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Jilio Bwire, wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu yaliyofanyika wilayani Nyamagana ambapo amesema kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kuwalinda walemavu, lakini bado vitendo vya mauji dhidi yao, hasa wenye ulemavu wa ngozi (albino) vimeonekana bado kuendelea nchini.
Aidha, Bwire aliyataja baadhi ya matatizo yanayowakabili walemavu kuwa ni pamoja na kubaguliwa,
miundombinu kutokuwa rafiki kwao, ukosefu wa maeneo ya biashara, shule maalum za walemavu pamoja na bajeti maalumu kutoka serikalini.
Mbali na hayo Bwire aliiomba Serikali iwafungulie vyuo vya ufundi ili waweze kupata mafunzo na kutumia elimu hiyo kufanya biashara ili kuondokana na utegemezi.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kitengo cha walemavu, Jelia Mtani, alisema Serikali inatambua watu wenye ulemavu na imeweka bajeti kwa ajili ya kuwahudumia watu hao.
Kuhusu walemavu wasioona, alitaka wakumbukwe pia katika suala zima la uchaguzi ambapo mara nyingi huwa hawapati haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi.
“Tusiwatenge watu hawa kwani nao ni kama watu wengine, tuwape haki yao ya kikatiba, nao wana haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka,” alisisitiza Mtani.
Maadhimisho hayo yalishirikisha walemavu kutoka wilaya za Sengerema, Magu, Misungwi, Ukerewe, Ilemela, Kwimba na Nyamagana, yakiwa na kaulimbiu inayosema “Maendeleo endelevu ni ahadi ya teknolojia.”
Lengo letu ni kuhakikisha unapata story zote kila kona ya Tanzania, tafadhali endelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com kwa habari zaidi kila siku
No comments:
Post a Comment