Showing posts with label Mwanza. Show all posts
Showing posts with label Mwanza. Show all posts
WANANCHI WAASWA KUCHAGUA VIONGOZI WAPENDA MAENDELEO
Mwanza, Na Goodluck Ngowi
Wananchi wametakiwa kujenga tabia ya kuchagua viongozi walio na sifa ambao wanapenda maendeleo ya wananchi bila kujali maslahi yao binafsi kama ilivyo kwa baadhi ya viongozi hivi sasa.
Hayo yamebainishwa katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mwishoni mwa wiki iliyopita katika uwanja wa Mahina kati, ambapo Diwani wa kata ya Mahina, Charles Chinchibela aliwasihi wananchi kuepukana na wanasiasa wa kwenye kahawa.
“Epukaneni na wanasiasa wanaozungumza siasa za kwenye kahawa, ambapo kila mtu anajifanya mjuaji kumbe hajui sikilizeni siasa za maendeleo ambazo zitawasaidia ndani ya miaka mitano”. Alisema Chinchibela
Mbali na hayo, diwani huyo alisema kuwa, wananchi wanapaswa kuwa makini na viongozi wadanganyifu wanaodai kuwa yeye hajafanya kitu, huku wakijua kuwa uchaguzi huu mdogo ndio taswira ya uchaguzi mkuu wa mwakani.
Naye, mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti katika eneo hilo la Mahina kati Pascal Bulabo aliwataka wananchi hao kumpigia kura siku ikifika ili kuleta maendeleo yaliyoshindwa kuletwa na chama tawala.
“CCM wameshindwa kwa miaka yote hiyo kuleta maendeleo, imefika wakati kwa wakazi wa Mahina kuchagua CHADEMA, kwa kuwa ni chama kinachopenda maendeleo kwa watu wake”. Alisema Bulabo.
Endelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com kwa kupata habari zaidi, nasi tunaahidi kuwa nawe kila iitwapo leo.
WADAU WA KEMIKALI NCHINI WATAKIWA KUZINGATIA MATUMIZI SAHIHI
Mwanza, Na Goodluck Ngowi
Wadau wa kemikali za viwandani na majumbani wamehimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya bidhaa hiyo kwa lengo la kuepusha madhara kwa binadamu na mazingira.
Hayo yameelezwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa wasajiliwa wapya 106 wa matumizi ya kemikali Kanda ya Ziwa, iliyofanyika kwenye hoteli ya JB
Belmonte jijini Mwanza.
Profesa Manyele, alisema Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani namba 3 ya mwaka 2003 inalenga kulinda afya za binadamu na mazingira dhidi ya matumizi mabaya ya kemikali na ajali.
“Kemikali zisipotumika kwa uangalifu zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira, hivyo kwa kuzingatia sheria hii tutaepusha madhara kwa afya za Watanzania na mazingira
yanayowazunguka,” alisema Profesa Manyele.
Aidha, aliendelea kusema kuwa faida za kusajili matumizi ya kemikali ni pamoja na kutambua aina za bidhaa hiyo na madhara yake kwa afya ya binadamu na mazingira, huku akiwataka wazalishaji, waagizaji, wasafirishaji na watumiaji wa kemikali na wananchi kwa jumla kutumia ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupata ushauri juu ya matumizi shahihi ya bidhaa hiyo.
Kwa upande wao wadau na viongozi wa kampuni zilizopewa vyeti hivyo waliishukuru ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwapatia usajili huo baada ya kutimiza masharti.
Naye Meneja wa kampuni ya Atlas Copco iliyopo jijini hapa, Laurent Francis, alisema wakemia wametambua kuwa wamefikia kiwango kinachotakiwa ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira.
Ni kila iitwapo leo tupo pamoja nawe kwa lengo moja tu, ambalo ni kuhabarishana mambo mbalimbali yanayotokea katika kila kona ya nchi hii, tambua kuwa tunathamini sana uwepo wako wewe msomaji wetu, tafadhali endelea kuwa nasi.
WALEMAVU WAOMBA KUTONYANYAPALIWA
Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) Mkoa wa Mwanza, wameiomba Serikali kutowanyanyapaa, badala yake wawajali kwa kuwatimizia mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na elimu.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Jilio Bwire, wakati wa maadhimisho ya siku ya walemavu yaliyofanyika wilayani Nyamagana ambapo amesema kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kuwalinda walemavu, lakini bado vitendo vya mauji dhidi yao, hasa wenye ulemavu wa ngozi (albino) vimeonekana bado kuendelea nchini.
Aidha, Bwire aliyataja baadhi ya matatizo yanayowakabili walemavu kuwa ni pamoja na kubaguliwa,
miundombinu kutokuwa rafiki kwao, ukosefu wa maeneo ya biashara, shule maalum za walemavu pamoja na bajeti maalumu kutoka serikalini.
Mbali na hayo Bwire aliiomba Serikali iwafungulie vyuo vya ufundi ili waweze kupata mafunzo na kutumia elimu hiyo kufanya biashara ili kuondokana na utegemezi.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kitengo cha walemavu, Jelia Mtani, alisema Serikali inatambua watu wenye ulemavu na imeweka bajeti kwa ajili ya kuwahudumia watu hao.
Kuhusu walemavu wasioona, alitaka wakumbukwe pia katika suala zima la uchaguzi ambapo mara nyingi huwa hawapati haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi.
“Tusiwatenge watu hawa kwani nao ni kama watu wengine, tuwape haki yao ya kikatiba, nao wana haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka,” alisisitiza Mtani.
Maadhimisho hayo yalishirikisha walemavu kutoka wilaya za Sengerema, Magu, Misungwi, Ukerewe, Ilemela, Kwimba na Nyamagana, yakiwa na kaulimbiu inayosema “Maendeleo endelevu ni ahadi ya teknolojia.”
Lengo letu ni kuhakikisha unapata story zote kila kona ya Tanzania, tafadhali endelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com kwa habari zaidi kila siku
WATOTO WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU WAFANYIWA TOHARA
Mwanza, Na Goodluck Ngowi
Shirika lisilo la kiserikali la New Dream for Community Change Organization (NEDCO) mkoani Mwanza limefanikiwa kuwafanyia watoto wanaoishi katika mazingira magumu tohara na wengine kuwarudisha kwao.
Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa shirika hilo, Shabani Mkama, alisema kuwa tohara hiyo walifanya kwa kushirikiana na hospitali ya Mkoa wa wa Mwanza Sekoutoure baada ya kugundua kuwepo kwa watoto ambao hawajafanyiwa tohara mitaani.
“Kwa kushirikiana na hospitali ya Mkoa Sekeoutoure tumefanikiwa kuwafanyiwa watoto watano tohara ikiwa ni kazi mojawapo ya jamii inayotupasa kufanya”alisema Mkama.
Shirika hilo pia limefanikiwa kuanzisha timu ya mpira wa miguu kwa watoto wa mitaani kupitia wadhamini wa makampuni mbalimbali ikiwemo kampuni ya vinywaji baridi ya Cocacola pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
“ jukumu la kuwalea watoto hao si la Serikali na mashirika pekee yake, bali ni jukumu la jamii nzima ”aliongeza Mkama
Ameongeza kuwa kupitia serikali ya mtaa wa mbugani A chini ya mwenyekiti Bernad Wegoro na diwani wa kata ya Mbugani mheshimiwa Hassan Kijuu wamefanikisha kuwasaidia watoto wa mitaani kupata sehemu ya kulala.
Mbali na hayo, Bwana Shabani amesema kuwa kuna changamoto wanazokumbana nazo ambazo ni pamoja na mitizamo finyu kwa wanajamii juu ya watoto wa mitaani, wazazi kutokubali kuishi na watoto hao kwa kusema kwamba tayari wana tabia za mitaani, upungufu wa rasilimali fedha, migogoro ya kifamilia pamoja na kuvunjika kwa ndoa na umasikini.
Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo wa NEDCO amewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo
kujitokeza na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shirika hilo katika kuisaidia jamii juu ya masuala mbalimbali.
WAFANYAKAZI WA SEKTA YA MADINI WASHAURIWA KUJIUNGA NA TAMICO
Mwanza, Na Goodluck Ngowi
Wafanyakazi katika sekta za ujenzi, nishati na migodi wameshauriwa kujiunga na matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi nyingine (TAMICO) kwa lengo la kuweza kupata haki zao za msingi ikiwemo mikataba inayokidhi matakwa ya kisheria.
Wito huo umetolewa jana jijini Mwanza na Katibu wa TAMICO Kanda ya ziwa, Joseph Mang'ana, ambaye alisema licha ya kuwepo kwa wafanyakazi wengi katika sekta hizo ni wafanyakai 1,495 pekee ndio waliojiandikisha katika chama hicho.
"Kwa mujibu wa takwimu tulizonazo kuna wafanyakazi wasiopungua 5,000 katika sekta hizi za nishati, madini na migodi lakini ni idadi ndogo waliojiandikisha, hali inayowakosesha faida mbalimbali kama mafunzo ya haki zao za msingi, kutetewa na wanasheria na mawakili wetu pindi wanapoachishwa kazi na kunyanyaswa na waajiriwa wao" alisema Mang’ana.
Aidha, Mang'ana aliwashauri waajiri hasa wa makampuni ya ujenzi kuhakikisha wanawapa wafanyakazi wao mikataba ya kudumu na kuweka mazingira bora ya kazi kwa wafanyakazi hao kama inavyoelekezwa na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazinini.
Mbali na hayo, Mang'ana alisema faida nyingine za kujiunga na TAMICO ni kupata haki ya kuchagua viongozi na kuchaguliwa kama wawakilishi wa chama hicho katika matawi maeneo yao ya kazi.
Asante kwa kuendelea kuifanya habarimkusanyiko.blogspot.com kuwa sehemu yako ya kupata habari tafadhali endelea kuwa nasi na tunadhamini sana uwepo wako kwetu.
NIMEKUWEKEA HAPA PICHA ZA MAFURIKO YALIYOTOKEA JIJINI MWANZA DISEMBA 2
Mwanza, Na Goodluck Ngowi
Hivi ndivyo hali ilivyokuwa kwa wakazi wa mtaa mabatini jijini Mwanza siku ya Disemba 2 baada ya mvua kubwa kunyesha kuanzia majira ya asubuhi na kusababisha na mafuriko.
Mwandishi wetu wa habarimkusanyiko.blogspot.com Goodluck Ngowi, ambaye anatuwakilisha mkoani humo, aliarifu kuwa mvua hiyo ilisababisha mto Mirongo kujaa maji na baadaye kuanza kutapisha maji kuelekea katika maeneo ya makazi ya watu.
Wakazi wa jijini Mwanza waliokubwa na mafuriko hayo wakijaribu kutoa mifuko ya takataka iliyosombwa na maji kuletwa kwenye makazi yao
Hivi ndivyo hali ilivyokuwa kwa wakazi wa mtaa mabatini jijini Mwanza siku ya Disemba 2 baada ya mvua kubwa kunyesha kuanzia majira ya asubuhi na kusababisha na mafuriko.
Mwandishi wetu wa habarimkusanyiko.blogspot.com Goodluck Ngowi, ambaye anatuwakilisha mkoani humo, aliarifu kuwa mvua hiyo ilisababisha mto Mirongo kujaa maji na baadaye kuanza kutapisha maji kuelekea katika maeneo ya makazi ya watu.
Kijana akitoa matope yaliyokuwa yameingia ndani ya nyumba yao baada ya mvua kubwa kunyesha
Wakazi wa jijini Mwanza waliokubwa na mafuriko hayo wakijaribu kutoa mifuko ya takataka iliyosombwa na maji kuletwa kwenye makazi yao
Sehemu hii ya vinywaji (Bar) pia ilikubwa na sakata hilo la mafuriko
Watoto wakishangaa namna bar hii ilivyovurugika kutokana na mafuriko
Unastahili kupata matukio na habari zote kila zinapotokea na hilo ni jukumu letu sisi, hivyo endelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com upate mengi zaidi.
UJENZI WA MAABARA WAVURUGA VIONGOZI MWANZA
Muonekano wa jiji la Mwanza mjini
Mwanza, Na Goodluck NgowiUjenzi wa vyumba vya maabara umeonekana kuwavuruga baadhi ya viongozi wilayani Ilemela mkoani Mwanza baada ya suala hilo kugubikwa na migogoro ya ardhi, jambo lililosababisha kushindwa kukamilika kwa maabara katika shule ya sekondari Kirumba na Kibuhoro kukwama.
Kukwama kwa ujenzi huo kumetokana na baadhi ya wananchi wilayani humo kufungua kesi mahakamani na kulalamika kwamba, hawajalipwa fidia zao zakuhamishwa kutoka eneo hilo, jambo lililomshangaza Mkuu wa Mkoa huo, Magesa Mulongo.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa maabara, Kaimu Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Justini Lukaza, alisema kesi ya viwanja hivyo iko mahakamani tangu mwaka 2005.
“Wakati wilaya yetu inazaliwa mwaka 2012 mgogoro tayari ulikuwepo, kwa hiyo bado tunaendelea nao, ili kupata muafaka wa kupata eneo la kujenga maabara hizi kwa sababu sisi lengo letu ni kujenga vyumba vya maabara 72 na vilivyokamilika ni 17, lakini 22 viko katika hatua ya lenta na vingine 20 vipo katika hatua ya msingi, huku 4 vikiwa katika hatua ya boma, 2 vikifikia hatua ya kuezekwa na vingine 7 havijajengwa,” alisema Lukaza.
Kutokana na hali hiyo, Mulongo alimtaka Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Steve Singira, kujibu kesi ya mgogoro huo uliosababishwa kutojengwa kwa maabara ili kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Kwa upande wake Singira alisema, anashughulikia kesi hiyo kwa kushirikiana na maofisa wengine wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
“Hii haiwezekani, Novemba 30 maabara hazijajengwa na wewe unasema ni Mkurugenzi, nasema lazima ile kwa mtu kabla haijala kwangu, nidanganyeni tu, sio kwamba kesi iko mahakamani ila mmeshindwa kujenga maabara za watoto shuleni. Wewe mwanasheria kazi yako ni ipi kama mpaka leo kesi haijaisha na wewe upo tu unakula raha? Alihoji Mulongo na kuongeza kuwa, “Mwanasheria unasema wamelipwa fidia na nani? Kuna makubaliano yoyote
ya ushahidi yanayoonyesha malipo ya watu hao, mnataka kutueleza kwamba watoto wanafungua shule Januari hakuna maabara kwa sababu kesi itakamilika mwezi huo?” aliendelea kuhoji Mulongo.
Mbali na hayo Mulongo pia aliwaonya wahasibu na wachumi wa halmashauri hiyo juu ya ucheleweshwaji wa fedha za kugharimia ujenzi wa maabara hizo.
“Yaani mtu yuko tu ofisini, pengine hawa watendaji wanakuja kila siku hapa kuuliza fedha hazipo wakati huo mtu amekaa wakati kazi yake ni kusaini hundi tu, lakini mpaka iwe usumbufu, acheni roho mbaya,”
alisema Mulongo.
Asante kwa kuendelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com, tafadhali endelea kuungana nasi kwa habari zaidi kila siku.
Subscribe to:
Posts (Atom)








