Muonekano wa jiji la Mwanza mjini
Mwanza, Na Goodluck NgowiUjenzi wa vyumba vya maabara umeonekana kuwavuruga baadhi ya viongozi wilayani Ilemela mkoani Mwanza baada ya suala hilo kugubikwa na migogoro ya ardhi, jambo lililosababisha kushindwa kukamilika kwa maabara katika shule ya sekondari Kirumba na Kibuhoro kukwama.
Kukwama kwa ujenzi huo kumetokana na baadhi ya wananchi wilayani humo kufungua kesi mahakamani na kulalamika kwamba, hawajalipwa fidia zao zakuhamishwa kutoka eneo hilo, jambo lililomshangaza Mkuu wa Mkoa huo, Magesa Mulongo.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa maabara, Kaimu Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Justini Lukaza, alisema kesi ya viwanja hivyo iko mahakamani tangu mwaka 2005.
“Wakati wilaya yetu inazaliwa mwaka 2012 mgogoro tayari ulikuwepo, kwa hiyo bado tunaendelea nao, ili kupata muafaka wa kupata eneo la kujenga maabara hizi kwa sababu sisi lengo letu ni kujenga vyumba vya maabara 72 na vilivyokamilika ni 17, lakini 22 viko katika hatua ya lenta na vingine 20 vipo katika hatua ya msingi, huku 4 vikiwa katika hatua ya boma, 2 vikifikia hatua ya kuezekwa na vingine 7 havijajengwa,” alisema Lukaza.
Kutokana na hali hiyo, Mulongo alimtaka Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Steve Singira, kujibu kesi ya mgogoro huo uliosababishwa kutojengwa kwa maabara ili kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Kwa upande wake Singira alisema, anashughulikia kesi hiyo kwa kushirikiana na maofisa wengine wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
“Hii haiwezekani, Novemba 30 maabara hazijajengwa na wewe unasema ni Mkurugenzi, nasema lazima ile kwa mtu kabla haijala kwangu, nidanganyeni tu, sio kwamba kesi iko mahakamani ila mmeshindwa kujenga maabara za watoto shuleni. Wewe mwanasheria kazi yako ni ipi kama mpaka leo kesi haijaisha na wewe upo tu unakula raha? Alihoji Mulongo na kuongeza kuwa, “Mwanasheria unasema wamelipwa fidia na nani? Kuna makubaliano yoyote
ya ushahidi yanayoonyesha malipo ya watu hao, mnataka kutueleza kwamba watoto wanafungua shule Januari hakuna maabara kwa sababu kesi itakamilika mwezi huo?” aliendelea kuhoji Mulongo.
Mbali na hayo Mulongo pia aliwaonya wahasibu na wachumi wa halmashauri hiyo juu ya ucheleweshwaji wa fedha za kugharimia ujenzi wa maabara hizo.
“Yaani mtu yuko tu ofisini, pengine hawa watendaji wanakuja kila siku hapa kuuliza fedha hazipo wakati huo mtu amekaa wakati kazi yake ni kusaini hundi tu, lakini mpaka iwe usumbufu, acheni roho mbaya,”
alisema Mulongo.
Asante kwa kuendelea kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com, tafadhali endelea kuungana nasi kwa habari zaidi kila siku.
No comments:
Post a Comment