Mwanza, Na Goodluck Ngowi
Wadau wa kemikali za viwandani na majumbani wamehimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya bidhaa hiyo kwa lengo la kuepusha madhara kwa binadamu na mazingira.
Hayo yameelezwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa wasajiliwa wapya 106 wa matumizi ya kemikali Kanda ya Ziwa, iliyofanyika kwenye hoteli ya JB
Belmonte jijini Mwanza.
Profesa Manyele, alisema Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani namba 3 ya mwaka 2003 inalenga kulinda afya za binadamu na mazingira dhidi ya matumizi mabaya ya kemikali na ajali.
“Kemikali zisipotumika kwa uangalifu zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira, hivyo kwa kuzingatia sheria hii tutaepusha madhara kwa afya za Watanzania na mazingira
yanayowazunguka,” alisema Profesa Manyele.
Aidha, aliendelea kusema kuwa faida za kusajili matumizi ya kemikali ni pamoja na kutambua aina za bidhaa hiyo na madhara yake kwa afya ya binadamu na mazingira, huku akiwataka wazalishaji, waagizaji, wasafirishaji na watumiaji wa kemikali na wananchi kwa jumla kutumia ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupata ushauri juu ya matumizi shahihi ya bidhaa hiyo.
Kwa upande wao wadau na viongozi wa kampuni zilizopewa vyeti hivyo waliishukuru ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwapatia usajili huo baada ya kutimiza masharti.
Naye Meneja wa kampuni ya Atlas Copco iliyopo jijini hapa, Laurent Francis, alisema wakemia wametambua kuwa wamefikia kiwango kinachotakiwa ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira.
Ni kila iitwapo leo tupo pamoja nawe kwa lengo moja tu, ambalo ni kuhabarishana mambo mbalimbali yanayotokea katika kila kona ya nchi hii, tambua kuwa tunathamini sana uwepo wako wewe msomaji wetu, tafadhali endelea kuwa nasi.
No comments:
Post a Comment