WATOTO WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU WAFANYIWA TOHARA



Mwanza, Na Goodluck Ngowi
Shirika lisilo la kiserikali la New Dream for Community Change Organization (NEDCO) mkoani Mwanza limefanikiwa kuwafanyia watoto wanaoishi katika mazingira magumu tohara na wengine kuwarudisha kwao.

Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa shirika hilo, Shabani Mkama, alisema kuwa tohara hiyo walifanya kwa kushirikiana na hospitali ya Mkoa wa wa Mwanza Sekoutoure baada ya kugundua kuwepo kwa watoto ambao hawajafanyiwa tohara mitaani.

“Kwa kushirikiana na hospitali ya Mkoa Sekeoutoure tumefanikiwa kuwafanyiwa watoto watano tohara ikiwa ni kazi mojawapo ya jamii inayotupasa kufanya”alisema Mkama.

Shirika hilo pia limefanikiwa kuanzisha timu ya mpira wa miguu kwa watoto wa mitaani kupitia wadhamini wa makampuni mbalimbali ikiwemo kampuni ya vinywaji baridi ya Cocacola pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

“ jukumu la kuwalea watoto hao si la Serikali na mashirika pekee yake, bali ni jukumu la jamii nzima ”aliongeza Mkama

Ameongeza kuwa kupitia serikali ya mtaa wa mbugani A chini ya mwenyekiti Bernad Wegoro na diwani wa kata ya Mbugani mheshimiwa Hassan Kijuu wamefanikisha kuwasaidia watoto wa mitaani kupata sehemu ya kulala.

Mbali na hayo, Bwana Shabani amesema kuwa kuna changamoto wanazokumbana nazo ambazo ni pamoja na mitizamo finyu kwa wanajamii juu ya watoto wa mitaani, wazazi kutokubali kuishi na watoto hao kwa kusema kwamba tayari wana tabia za mitaani, upungufu wa rasilimali fedha, migogoro ya kifamilia pamoja na kuvunjika kwa ndoa na umasikini.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo wa NEDCO amewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo
kujitokeza na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shirika hilo katika kuisaidia jamii juu ya masuala mbalimbali.


No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname