KENGE WAMPONZA RAIA WA KUWAIT



Jeshi la Polisi la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) linamshikilia raia wa Kuwait kwa tuhuma za kukutwa na viumbe hai aina ya Kenge 149 wenye thamani ya Shilingi milioni 6.3.

Kamanda wa Polisi wa JNIA, Khamis Suleiman alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Hussain Ahmed Ally Mansour (34), raia wa Kuwait ambaye alikamatwa uwanjani hapo jana majira ya saa 5 usiku wakati alipokuwa akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Kuwait kupitia Dubai na Shirika la Ndege la Emirates .

Aidha, Kamanda Selemani alisema Mansour alikamatwa na wanyama hao ambao aliwahifadhi kwenye mifuko midogo midogo ilivyowekwa katika begi kubwa lenye rangi nyeusi.

“Kenge waliwekwa kwenye mifuko midogo midogo 15 na kila mmoja kuna kenge 15 na mifuko mingine walikaa wawili,” alisema kamanda Selemani.

Hata hivyo, kamanda alisema kati ya kenge hao, 15 walikufa na walio hai walikuwa 134 ambao walikuwa wamefichwa kwenye mifuko hiyo.

Kamanda Seleman aliendelea kusema wakati wanafanyiwa upekuzi ndipo walipogundua kuna vitu ambavyo vinafanana na nyoka na kuamua kuwashirikisha wataalam wa maliasili ambao walibaini kuwa begi hilo lilikuwa na Kenge.

“Huyu mtuhumiwa alikuja nchini Januari 6, alitiliwa mashaka na Polisi wa JNIA na tulimuamuru akae pembeni kwa upekuzi zaidi na kugundua anasafirisha kenge bila kibali,”alisema Selemani.

Pamoja na hayo, Kamanda Selemani alisema walipoendelea kumuhoji mtuhumiwa huyo alidai kuwa alikuja nchini kwa ajili ya kuchukua viumbe aina ya ndege, lakini baada ya kuwakosa aliamua kubeba kenge hao.

Sambamba na hayo Kamanda Selemani alitoa wito kwa wananchi kuwa na uzalendo wa nchi yao wanapoona mtu anasafirisha rasilimali za nchi watoe taarifa katika Jeshi la Polisi. Huku akisema kwamba Polisi wataendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege ili kudhibiti aina hiyo ya utoroshaji wa nyara.

Asante kwa kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com, tafadhali endelea kuwa nasi.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname