KILIMO NA VIWANDA VYAELEZWA KUWA SULUHISHO LA TATIZO LA AJIRA KWA VIJANA



MBUNGE wa jimbo la Nzega kupitia tiketi ya (CCM),Dr Khamis Kigwangalla amesema kuwa ili
kutatua tatizo la ajira kwa vijana nchini Serikali inatakiwa kuwekeza kwenye kilimo na Viwanda.

Hayo aliyasema alipokuwa akizungumza katika mdahalo wa vijana, wanasiasa wa vyama mbalimbali
Jijini Mwanza, ambapo Dr Kigwangala alisema kuwa njia pekee ya kutatua tatizo la ajira kwa vijana ni kuwekeza katika sekta ya kilimo na kufufua viwanda vilivyotelekezwa.

“katika kutatua hili tatizo la ajira kwa vijana Serikali inatakiwa kuwekeza na kuongeza nguvu kwenye sekta ya kilimo na viwanda ambavyo vingine vimeshatelekezwa”, alisema Kigwangalla

Aidha, aliongeza kuwa mbali na kuwekeza katika kilimo pia serikali inapaswa kuwekeza kwenye misingi ya kuwajengea uwezo vijana na kuzalisha kwa kuanzisha Mfuko wa vijana na Bank ya vijana itakayowapa fursa ya kupata mikopo na kujiajiri wenyewe.

Mbali na hayo Dr Kigwangala alisema kuwa kwa sasa Serikali ya Tanzania haipaswi kutegemea gesi kama njia ya kuondoa umasikini na kuacha kutegemea kilimo ambacho ndicho chenye uhakika wa kuwaondoa Watanzania katika umasikini na ukosefu wa ajira.

Kuhusiana na suala hilo la gesi Dr Kigwangala alisema gesi ya Tanzania haitasaidia kukabiliana na umasikini kutokana na mikataba iliyopo ambayo ni mibovu, huku akiongeza kuwa gesi ambayo
wazawa hawajapewa fursa ya kuwekeza itayonufaisha mataifa ya Ulaya na sio Watanzania.

"Binafsi siridhiki na mikataba iliyopo maana haikuwa wazi mpaka sasa na masharti ya kwenye mikataba haikujadiliwa kwa uwazi wakati kulikuwa hakuna sera wala sheria ya gesi ambayo ilipaswa kutoa Muongozo", alisema Kigwangalla


Aidha, akijibu swali kuhusu umri wa mgombea wa urais pamoja na nia yake ya kugombea urais ifikapo Julai mwaka huu, Kigwangala alisema kuwa sio sahihi watu wa chini ya miaka 40 kunyimwa fursa ya kugombea Urais.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa watu wenye umri wa chini ya miaka 40 wanapewa fursa ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa katiba hivyo hawana budi kupewa fursa ya kuchaguliwa hata katika ngazi ya Rais kwa vile ni haki zenye uzito sawa.
 Habari hii imeandikwa na kuletwa kwenu na mwakilishi wetu wa habarimkusanyiko blog Godluck Ngowi kutoka Jijijni Mwanza

Asante kwa kutembelea habarimkusanyiko.blogspot.com, tambua kuwa tunathamini sana uwepo wako msomaji wetu tafadhali endelea kuwa nasi kila iitwapo leo

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname