OJADACT YAMTAKA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUFUPISHA MUDA WA KUFUATILIA MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI NCHINI



WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, ametakiwa kufupisha muda alioutangaza kwa kikosi alichokiteua kufatilia mauaji ya albino katika mikoa ya kanda ya ziwa, ambacho alikipa muda wa wiki mbili.


Akizungumza na wanahabari ofisini kwake, Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wa kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu nchini (OJADACT), Edwini Soko alisema kuwa suala la uhai wa mtu halihitaji subira kama kwenda kutoa posa.

“OJADACT tunamtaka waziri wa mambo ya ndani afupishe muda wa wiki mbili alioutangaza kwa kikosi kazi alichokiteua kufuatilia mauaji ya albino, suala la uhai wa mtu halihitaji subira kama ya kwenda kutoa posa,” alisema Soko.

Soko alisema kuwa OJADACT imesikitishwa sana na tukio la utekwaji wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Pendo Emmanuel (4) ambaye kimsingi hadi leo hajapatikana na kudai ni kinyume cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 14.

Pendo Emmanuel (4) alitekwa Disemba 27, mwaka jana katika kijiji cha Ndami, wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Sambamba na hayo, Soko alitumia nafasi hiyo kuiomba jamii, vyombo vya dola na taasisi nyingine kushiriki kwa namna mbalimbali kusaidia kupatikana kwa mtoto huyo na si vyema kuliacha suala hilo kwa Jeshi la Polisi peke yake.
Habari hii imeandikwa na kuandaliwa na Goodluck Ngowi, mwakilishi wa habarimkusanyiko.blogspot.com kutoka jijini Mwanza, tafadhali endelea kuwa nasi msomaji wetu.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname