PAPA FRANCIS AITAKA UFILIPINO KUPAMBANA NA RUSHWA



Kumbe suala la tatizo la rushwa si hapa nchini tu, ni tatizo ambalo pia linalikabili Serikali ya Ufilipino, ambapo kufuatia tatizo hilo kukithiri nchini Ufilipino Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, ameitaka Serikali ya nchi hiyo kupambana na tatizo hilo lililokithiri nchini humo, huku akiwataka viongozi pia kumaliza kabisa umaskini.


Papa Francis ametoa wito huo, katika hotuba yake ya kwanza wakati wa ziara yake ya siku tano nchini Ufilipino, ambapo amesema umefika wakati kwa viongozi wa kisiasa kuzingatia uadilifu, uaminifu na kujitolea kwa maslahi ya watu wote, na kusikia kilio cha mamilioni ya wananchi wake walio maskini na hivyo kuleta haki sawa za kijamii.

''Wasaidieni wale wanaoishi katika jamii iliyoathirika kwa umaskini na rushwa, waliokata tamaa ya kiroho, wanaokuwa kwenye majaribu ya kutaka kuacha shule na kuishi mitaani. Wafilipino wanajulikana kila mahali kwa upendo wao kwa Mungu, na kujitoa kwao kwa Mama Maria pamoja na Rozari yake,” alisema Papa Francis.

Aidha, papa amewasihi wananchi wote wa Ufilipino na katika ngazi zote kukataa aina yoyote ya rushwa, ambayo inachangia kuchukua rasilimali kutoka kwa watu maskini. Huku akisema kwamba inawapasa watu kuondokana na ukandamizaji na dhuluma, ambavyo kwa pamoja husababisha kutokuwepo kwa haki sawa miongoni mwa jamii.

Inaelezwa kuwa tatizo la rushwa limekuwa likiikumba Ufilipino tangu enzi za utawala wa miaka 20 wa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo, Hayati Ferdinand Marcos, ambaye pamoja na mkewe, aliyekuwa akipenda maisha ya kifahari, walituhumiwa kuiba kati ya Dola bilioni tano na Dola bilioni kumi, kabla hawajaondolewa madarakani mwaka 1986.

Hata hivyo Rais Aquino mtetezi wa demokrasia na mtoto wa rais wa zamani wa Ufilipino, Corazon Aquino, aliingia madarakani mwaka 2010, huku akiahidi kuwa na serikali yenye uwazi, utawala bora pamoja na kupambana na tatizo la rushwa kwa lengo la kuwatoa Wafilipino katika dimbwi la umaskini.
Baadhi ya picha za mapokezi ya Papa Francis inchini Ufilipino.
Rais Benigno Aquino wa Ufilipino, akisalimiana na Papa Francis

Papa Francis akiwapungia mkono watu waliofurika kumlaki, Manila
Watu wakipunga mikono kumsalimu Papa, Manila
Katika ziara yake hiyo Papa Francis alikutana na Rais Aquino, pamoja na kuongoza Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Manila. Baada ya Ibada hiyo, Papa Francis alikutana na watoto wa mitaani, ambapo alitumia muda wa dakika 20 kuwasikiliza, kuimba pamoja nao na kubadilishana zawadi.

Taarifa zinaeleza kuwa hapo baadaye leo, Papa Francis atakutana na familia za Wafilipino, huku kesho akiitumia kwenda kwenye jimbo la mashariki la Leyte, ambapo anatarajiwa kukutana na kuwafariji wahanga wa kimbunga Haiyan, kilichoikumba nchi hiyo mwaka 2013. Kimbunga hicho kilisababisha vifo vya zaidi ya watu 7,300 na kuviangamiza kabisa vijiji kadhaa.

Katika ziara hiyo ya Papa Francis nchini humo, ulinzi mkali umeimarishwa, ambapo kiasi cha wanajeshi na askari polisi 50,000 wametawanywa. Huku Rais Aquino akimueleza Papa kuwa ulinzi kama huo haujawahi kutokea nchini humo.
Source: DW

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname