SERIKALI YAAGIZA VIVUKO VYOTE NCHINI KUTUMIA TIKETI ZA KIELEKTRONIKI



SERIKALI imeagiza vivuko vyote nchini vitumie tiketi za mfumo wa kielectroniki ambao umeonesha mafanikia makubwa katika udhibiti na ukusanyaji mapato.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli wakati alipokuwa akizinduzi mashine ya ukataji tiketi kwa njia ya mfumo huo katika kivuko cha Kigongo-Busisi jana Kijijini Kigongo, wilayani Misungwi.

Waziri Magufuli pia aliagiza kivuko hicho kianze kutoa huduma saa 24, huku akisema kwamba mashine hizo zilifanyiwa majaribio katika kivuko cha Kigamboni jijini Dar es Salaam na zikaonesha ufanisi mkubwa.

“Nakuomba Chief Executive na Meneja wa Temesa wa kivuko hiki kianze kutoa huduma saa 24 usiku na mchana,…naagiza vivuko vyote nchini kuanzia Kahunda-Meisome, Lugezi-Kisorya hadi Mtwara na Dar, vyote vitumie mfumo huu.” Aliagiza.

Baada ya Kigamboni, wizara yake iliingia mkataba na kampuni ya Maxco ikafunga mashine hizo Kigongo-Busisi, Septemba mosi 2014 na zikaanza kutumika rasmi na hadi sasa umeonesha mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka mapato kwa asilimia 30 hadi 40 tofauti na wakati wa tiketi za kawaida.

“Njia ya kukomesha mwizi ni kwenda kisayansi, mfumo wa tiketi hizi ni mzuri, ulifanyiwa majaribio na kuza matunda, mapato ya awali yalikuwa kidogo sasa yameongezeka kwa kati ya asilimia 30 hadi 40,”
alisema Waziri Magufuli. Huku akiwataka walinzi (Suma JKT), kuwakamata wafanyakazi waliozoea kuiba mafuta.

Mbali na hayo, Waziri Magufuli pia alieleza kuwa, wizara yake inatarajia mfumo huo ulioongeza ufanisi wa mapato na kudhibiti wizi utaongeza kiwango cha makusanyo katika kivuko hicho na kufikia asilimia 5o.

Huku akishangiliwa kutokana na umahili wa kuzungumza lugha mbalimbali za kiasili, Magufuli aliuaagiza uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) pia kuhakikisha wanafunzi wote wanasafiri bure katika kivuko hicho na vingine vya Serikali ili wapate elimu bora na baadaye taifa lipate mafundi wa kujenga vivuko.

Alisema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Suma JKT, wizara yake itaendelea kutumia askari hao kulinda vivuko vingine vyote nchini na kuutaka uongozi wa Temesa kuboresha mafao ya wafanyakazi wake hususani wa kivuko hicho kinacholiingizia taifa fedha nyingi.

Hapo awali Mtendaji Mkuu wa Temesa, Marcellin Magesa alisema mradi huo wa Kigongo-Busisi ulisanifiwa na Temesa kwa lengo la kuboresha huduma za kivuko hicho zikidhi matakwa ya wananchi na kudhibiti mapato.

Aidha, Magesa alieleza kuwa, baada ya mfumo huo kukamilika walifanya matengenezo ya kuweka vifaa maalum vya kurekodi matukio yote yanayofanyika kivukoni hapo ambayo sasa yamekamilika, huku lengo likiwa ni kuboresha huduma na watumishi wake wafanye kazi kwa ufanisi.

Mbali na hayo, akimkaribisha Waziri Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Magessa Mulongo aliwaomba wananchi kupokea kwa mikono miwili mfumo huo ambao Serikali imeubuni ili huduma zake ziende na wakati na kuwaondolea usumbufu.
Hizi ni baadhi ya picha za vivuko mbalimbali vinavyotumika hapa nchini







Habari hii imeandaliwa na kuletwa kwako na Goodluck Ngowi, ambaye ni mwakilishi wa habarimkusanyiko.blogspot.com mwenye jukumu la kuhakikisha hupitwi na taarifa zote za jijini Mwanza na maeneo yake ya karibu, Asante kwa kuendelea kutuamini na kuwa nasi msomaji wetu

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname