ACHOMEWA NYUMBA NA KUFYEKEWA MASHAMBA KISA MALI ZA URITHI


MATUKIO ya uvunjaji wa sheria kwa kisingizio cha watu wenye hasira kali yameanza kuibuka tena wilayani Missenyi mkoani Mwanza baada ya watu kuteketeza nyumba mbili na kufyeka mashamba ya migomba.


Nyumba na mashamba hayo yaliyoteketezwa ni mali ya Azizi Ahmada, mkazi wa kijiji cha Nyabihokwe, kata ya Bwanjai, anayetuhumiwa kujihusisha na ujambazi.

Aidha, kufuatia tukio hilo wananchi walishangazwa na kitendo cha askari polisi kuwakamata baadhi ya watuhumiwa wa tukio hilo kisha kuwachia, huku wakivishauri vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza suala hilo kwa makini na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika.

Wananchi hao walisema kumekuwepo na mgogoro mkubwa wa kifamilia kuhusu urithi, ambapo baadhi ya ndugu wa Ahmada wamekuwa wakieneza uvumi kuwa ni jambazi, huku ikielezwa kuwa ndiye aliyerithishwa mali nyingi zaidi.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa kitongoji cha Bukomo, Revina Benjamin, alisema wakati wa tukio hilo alikuwa safari.

Hata hivyo, kwa upande wa Mwenyekiti wa kijiji cha Nyabihokwe, Jonathan Tibela, aliwatuhumu baadhi ya ndugu kuhusika na tukio hilo kwani mgogoro umekuwepo kati yao muda mrefu na kwamba hawezi kuthibitisha vitendo vya ujambazi. Huku akisema kuwa alichukua hatua ya kuitisha mkutano wa wakazi wa kitongoji hicho kusuluhisha mgogoro huo, lakini mahudhurio hayakutosha, hivyo aliahirisha mkutano.

Mbali na hayo, Ahmada alisema aliwatambua baadhi ya wanakijiji na ndugu zake waliomharibia mali zake, zikiwemo pikipiki mbili na kwamba vitendo vya ujambazi anavyosingiziwa ni kutokana na mgogoro wa mali kwani baba yao alizaa watoto sitini na yeye kugawiwa mali nyingi zaidi.
Habari hii imeandaliwa na Goodluck Ngowi ambaye ni mwandishi wa blog hii kwa upande wa jijini Mwanza. Asante kwa kuendelea kuwa nasi msomaji wetu.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname