MARUFUKU KUUZA VYAKULA OVYO, MAJI YA VIROBA, MATUNDA YALIYOMENYWA DAR ES SALAAM, SABABU NI KIPINDUPINDU
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiki amepiga marufuku biashara ya kuuza vyakula maeneo hatarishi ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
Maagizo hayo aliyatoa jana wakati akizungumzia hali ya kipindupindu jijini Dar es Salaam na kusema kuwa hadi kufikia jana kulikuwa na wagonjwa 56 ambao walibainika kuwa na dalili za ugonjwa huo wakitoka katika maeneo ya Makumbusho, Kijitonyama, Kimara, Sangara, Manzese, Kigogo, Tandale na Mwananyamala.
Pia ameagiza kupiga marufuku maji ya viroba maarufu kama maji ya Kandoro, matunda yaliyomenywa na juisi zilizotengenezwa kienyeji.
Mkuu huyo alisema wagonjwa waliopo katika kambi hadi kufikia jana walikuwa wagonjwa 36 na waliopata matibabu na kuruhusiwa ni wagonjwa 17 na kusema idadi ya vifo vya ugonjwa huo ni watu watatu. Aidha alisema ni marufuku kufanya shughuli za mazishi na kuweka matanga kwa familia zilizopoteza ndugu zao kwa ugonjwa huo.
“Nawataka viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa kata kupiga marufuku familia zilizokumbwa na ugonjwa huo kufanya shughuli za mazishi kwa ndugu zao na hata kuweka matanga,” alisema Sadiki.
Mkuu huyo alisema kutokana na wagonjwa wa kipindupindu kuongezeka wameanzisha kambi mpya kwa wagonjwa wapya wa ugonjwa wa kipindupindu Mbagala jijini Dar es Salaam ili kuepusha mlundikano wa wagonjwa katika kambi moja. Hadi sasa kuna kambi tatu zinazohudumia wagonjwa ikiwemo ya Mwananyamala Mburahati na Mbagala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment