Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki amekuwa mmoja wa mashuhuda, baada ya kujionea mabasi hayo alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam jana. Akizungumza baada ya kuyaona bandarini Dar es Salaam, alisema: “Tumefikia hatua nzuri na naipongeza Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDART) kwa kuleta mabasi hayo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma hii ya usafiri katika kipindi cha mpito.
Hii itasaidia kuondoa adha ya usafiri kwa wakazi wa jiji hili.” Alisema kampuni hiyo imepewa jukumu la kuendesha kipindi cha mpito ili waweze kupata uzoefu na zabuni ya mwendesha mradi kipindi cha kudumu itakapo tangazwa itasaidia wao kushindana.
Aliongeza kuwa, Serikali ilifanya kazi kubwa kuunganisha Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam na wamiliki wa daladala na baadaye kuanzisha kampuni ya UDART. Aidha alikanusha kuwa nauli za mabasi hayo imepangwa kuwa Sh 900 zilizotolewa katika mtandao, na kusema huo ni uzushi na upotoshaji na aliyefanya hivyo anatafutwa ili sheria ichukue mkondo.
Alisema suala la nauli linahusisha ushiriki wa taasisi mbalimbali chini ya Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) hivyo uzushi huo umewaletea usumbufu mkubwa wakazi wa Dar es Salaam hivyo wanatakiwa kuwapuuzia.
Msemaji wa Kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT), Sabri Mabrouk alisema mabasi yote yameingia yakiwemo ya meta 12 yapo 101 na meta 18 yapo 39 na huduma ya usafiri kipindi cha mipito itanza baada ya kukamilisha taratibu za bandari.
“Tuliahidi kuwa mwezi huu wa tisa mabasi yatakuwa yamewasili na ni kweli yamekuja,” na kwa pamoja na yale ya kufundishia yatakuwa mabasi 140,” alisema Mabrouk. Alifafanua kwamba mabasi hayo yametokea kiwandani China na yanakidhi miundombinu ya barabara. Mradi wa mabasi hayo unatarajia kuanza rasimi Oktoba 2 mwaka huu
No comments:
Post a Comment