ZIFAHAMU SABABU AMBAZO HUZUIA VIJANA WENGI KUTOFANIKIWA KATIKA MAISHA

Ikiwa tayari tumeingia ndani ya mwaka mpya 2016 na kila mtu tayari anayo mipango mipya na malengo ndani ya mwaka huu.

Lakini mipango yetu ya kimafanikio mara nyingi hurudishwa nyuma kutokana na fikra zetu wenyewe na kujikuta wengi tukiishia kulalama wenyewe au kuwalaumu watu wetu wa karibu na kuwaona kama ndio chanzo cha kurudisha nyuma mafanikio yetu.



Sasa leo naomba nikwambie kuwa kinachochangia na kuzuia mafanikio yetu ni baadhi ya tabia tulizo nazo.


Zingatia haya yafuatayo ikiwa unahitaji kufanikiwa katika maisha yako:- 

Epuka kufikiria sana juu ya makosa uliyoyafanya awali.

Kama kuna sehemu ulikosea katika siku za nyuma, hiyo imeshapita chukua hatu za kusonga mbele. Acha kutumia muda wako mwingi na kufikiri pale ulipokosea kwani hiyo haitakusaidia zaidi ya kukurudisha nyuma.

Kumbuka kuwa kukosea ni sehemu ya maisha ya binadamu, kitu cha msingi jifunze kutokana na hayo makosa uliyoyatenda siku za nyuma.

Usiwe mtu wa kuongelea ndoto zako kila siku.
Wengi wetu tumekuwa ni mahodari wa kuzungumza juu ya ndoto zetu, lakini sio watendaji. Kumbuka kuwa kama ni kuongea umeshaongea sana juu ya ndoto zako, umefika sasa wakati wa kutenda na unaweza kuanza kutenda kuanzia mwaka 2016 na ukafanikiwa kabisa.

Jenga tabia ya kuchukua hatua dhidi ya ndoto zako kila siku, hata kama ikiwa ni kwa kidogo kidogo ni lazima utasogea tu, mwisho utajikuta unafanikisha kile unachokitaka.

Usisubiri sana kutekeleza ndoto zako.
Kumbuka hakuna muda sahihi ambao upo wa kuanza kutekeleza ndoto zako kama unavyofikiria. Muda wa mafanikio na kufanya ndoto zako kuwa za kweli ni sasa na wala si kesho. Acha kuwa na tabia au fikra za kufikiri kuwa mipango yako mingi utaifanya siku nyingine. Anza kutekeleza mipango na malengo yako iliyojiwekea mara moja.
Tumia pesa zako vizuri.
Watu wengi huwa ni watumiaji wabaya wa pesa zao, lakini ni vyema ifahamike kwamba matumizi mabaya ya pesa, ni moja ya tabia kama tabia zingine, lakini ambayo ina nafasi kubwa ya kukukwamisha kwa kiasi kikubwa katika kufikia ndoto na malengo yako uliyojiwekea. Hivyo ili uweze kusonga mbele na kuachana na majuto uliyonayo jifunze kutunza pesa zako vizuri, utafanikiwa.

Epuka kuahirisha ahirisha mambo.
Ikiwa kuna jambo ulipaswa kulifanya leo, basi ni vizuri ukalifanya kuliacha na kutegemea utafanya kesho. Wakati wa kubadilisha maisha yako ni sasa na wala si kesho kama unavyofikiri.

Jiulize ni mara ngapi umesema utafanya kitu fulani kesho na hukufanya? Elewa kwamba tabia hiyo ni mbaya na itakuchelewesha sana kufanikiwa katika maisha.

Anza kujiwekea akiba.
Ikiwa huwa unashindwa kujiwekea akiba katika kipato katika pesa unayoipata basi jua kitakachokutokea katika maisha yako ni kushindwa kumudu kupata pesa ya kuendeshea miradi yako na mwisho wa siku utakuwa ni mtu wa kulalamika tu.

Kama unataka kuwa tajiri na kuwa huru kifedha anza kujifunza kujiwekea akiba, hii itakusaidia sana kusonga mbele katika mambo yako mengi.

Tambua ya kuwa mabadiliko yako yanategemea sana tabia yako ya kimaisha, hivyo anza kujiandaa kubadilika wewe kwanza ikiwa ni pamoja na kubadili hizo tabia ulizonazo ambazo zinakukwamisha sana. Kwa kadiri, utakavyoweza kumudu kubadili tabia zako kwa kiasi kikubwa, ndivyo utakavyo jikuta maisha yako yanakuwa na mafanikio makubwa kuliko unavyofikiri.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname