COASTAL UNION KUCHEZA NA AFC YA ARUSHA

 Vijana wa timu ya Coastal Union wakiwa katika mazoezi yao.
Timu ya soka ya Coastal Union ya jijini Tanga imepanga kusheherekea miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania kwa kucheza mechi ya kirafiki na timu ya AFC ya Arusha itakayochezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani Disemba 9 mwaka huu.

Mechi hiyo itakuwa ni miongoni mwa mechi za maandalizi kwa timu hiyo kwa lengo la kujiandaa na mechi zake za Ligi kuu soka Tanzania bara baada ya mapumziko ya siku 10 kutokana na Ligi kuu kusimama kwa muda ambapo itaendelea Disemba 26 mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari, Ofisa Habari wa Coastal Union, Oscar Assenga amesema kuwa mechi hiyo itakuwa ni muhimu kwa timu hiyo kujitayarisha kwa ajili ya raundi inayofuata kwenye michuano hiyo.

Aidha, ameongeza kuwa, baada ya kumalizika kwa mechi hiyo wataangalia uwezekano wa kutafuta mechi nyengine ya majaribio kabla ya kuanza ligi hiyo ambayo msimu huu imeonekana kuwa na upinzani mkubwa

Mbali na hayo, Assenga amesema kuwa timu hiyo ya AFC yenye makazi yake Mkoani Arusha inatarajiwa kuwasili mkoani Tanga Disemba 8, kwa ajili ya mtanange huo, huku lengo  likiwa ni kuziandaa timu zote mbili kwa mashindano yanayowakabili.

Sambamba na hayo, Assenga aliongeza kuwa, mechi hiyo ina umuhimu kwa timu zote mbili ikiwa ni pamoja na kujiandaa na Michuano ya Ligi kuu Tanzania bara raundi inayofuata na wapinzania wetu wanajiandaa na Ligi daraja la kwanza hapa nchini.

Hata hivyo amesema kuwa mazoezi ya timu hiyo yamekuwa yakiendelea kwa kasi kwenye viwanja vya Mkwakwani mjini humo, huku wachezaji wote waliokwenda mapumziko wakiwa tayari wamesharejea kikosini kwa asilimia kubwa.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname