MTOTO MWENYE ULEMAVU WA NGOZI ATEKWA MKOANI MWANZA



 
Watu wasiofahamika wamevunja nyumba na kisha kumteka mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino) na kutoweka naye kusikojulikana.

Tukiohilo la kusikitisha limetokea katika Kijiji cha Ndami, tarafa ya Mwamashimba wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, ambapo watu hao walivamia nyumba ya wazazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Pendo Emmanuel mwenye ulemavu huo wa ngozi. Huku wakiwa na mapanga na kisha kutoweka naye gizani baada ya kuwazidi nguvu wazazi wake.

Emmanuel Shilinde mzazi wa mtoto huyo ameieleza polisi kuwa majira ya saa nne usiku watu wawili waliuvunja mlango wa nyumba yake kwa jiwe na wakamchukua mtoto kwa nguvu kisha wakakimbilia gizani kwa pikipiki.

Aidha, Kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi mkoani mwanza Valentino Mlowola, amesema kuwa leo ni siku ya tatu tangu kutokea kwa tukio hilo na polisi bado ina matumaini ya kumpata akiwa hai mtoto huyo, kwa kuwa bado hawajaupata mwili wake akiwa amepoteza uhai.

Taarifa zinaendelea kusema kwamba msako unaendelea na tayari kuna watu watano wanazuiliwa na polisi ili kusaidia kufahamu mtoto huyo yuko wapi.

Takwimu za kuanzia mwaka 2006 zinaonyesha kuwa Albino 74 wameshauawa kikatili, huku 56 wakinusurika kifo, na kati yao 11 wamepata ulemavu mwingine wa kudumu.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname