Lebo ya kimataifa ya HIV/AIDS |
Maadhimisho hayo yanafanyika huku miito mbalimbali ikitolewa kwa ajili ya kutoa elimu na maarifa hasa kwa rika la vijana kuhusiana na maradhi ya UKIMWI. Hafla, mikutano na makongamano mbalimbali yanafanyika leo katika nchi mbalimbali ambapo lengo kuu ni kutoa tahadhari kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI.
Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka 2014 kitaifa yanafanyika mkoani Njombe, huku yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania bila maambukizo mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), Vifo vitokanavyo na UKIMWI, Ubaguzi na unyanyapaa inawezekana”
Nchini mwetu, ugonjwa huo uligundulika kwa mara ya kwanza mwaka 1981 mkoani Kagera, lakini kwa sasa umesambaa katika mikoa yote na umekuwa sababu ya vilio na majonzi makubwa kwenye jamii, pamoja na kusababisha vifo na kutuachia watoto yatima, wajane na wagane.
Mbali na hayo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) hivi karibuni walibainisha kuwa suala la unyanyasaji wa kijinsia limekuwa likichangia kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya virusi hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Valerie Msoka, amekemea vikali vitendo vya ubakaji, ukeketaji na ndoa za lazima ambavyo amesema, vinachangia kuenea maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Hadi sasa takwimu zinaonesha watu milioni 34 wanakadiriwa kuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi duniani, huku wengine milioni 35 wakiwa wameshafariki dunia katika maeneo mbalimbali ulimwenguni kutokana na maradhi hayo.
Nao mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF, umetoa wito wa kuweko uwekezaji zaidi katika kuwakinga na kuwatibu watoto.
Mbali na hayo, huko nchini Rwanda vyombo vya habari vimetakiwa kutoa elimu na kuleta uelewa kwa watu kuhusiana na UKIMWI.
Kwa upande wa nchini Uganda taarifa zinasema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wanaungana na walimwengu kuadhimisha siku ya ukimwi Duniani, huku kukiwa na ripoti kwamba, asilimia 60 ya vijana nchini humo hawana elimu na maarifa ya kutosha kuhusiana na namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi HIV.
Kila kukicha ni haki yako ya msingi sana kupata habari zilizotokea ndani na nje ya nchi na sehemu ya kupata yote hayo ni kupitia habarimkusanyiko.blogspot.com, tafadhari ungana nasi kila kukicha na tunasema asante kwa kutuunga mkono.
No comments:
Post a Comment