WATAKAOVURUGA TENA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA KUKIONA



Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema halitawaonea haya wale wote watakaosababisha kwa namna yoyote kuvuruga tena uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kurudiwa kesho katika baadhi ya maeneo.

Jumla ya mitaa 89 kutoka wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam, zinatarajiwa kufanya uchaguzi huo wa marudio kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi uliofanyika Desemba 14 mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari Kamishina wa Kanda Maalum, jijini Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova, amesema wamejipanga kila eneo kuhakikisha kuwa shughuli ya upigaji kura inafanyika kwa Amani.

“Vikosi vyetu viko salama vimejiandaa kukabiliana na fujo zozote zitakazoweza kujitokeza, naomba nieleweke kuwa polisi haitakuwa tayari kuwavumilia wale wote watakaosababisha vurugu, tunawachukulia hatua za kisheria,” alisema Kamishna Kova.

Aidha, Kamishna Kova alisema kwamba wametoa tahadhari hiyo kwa wananchi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa wakati wa zoezi hilo ili wasije wakajikuta wanaingia kwenye mgogoro bila sababu yeyote.

“Kutakuwa na askari waliovaa sare nadhifu, na askari wa kiraia ambao watakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa wakati wote amani inatawala katika vituo vya kupigia ,“ alisema Kamishna Kova.

Moja ya kasoro zilizopelekea kutofanya uchaguzi katika baadhi ya vituo ni kuchanganywa kwa majina ya wagombea wa uenyekiti na wajumbe.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname