BAADA YA UKIMYA KIASI KUHUSU UGONJWA WA EBOLA, HAYA NDIYO YANAYOENDELEA.



Taarifa zinasema kwamba wafanyakazi wa afya 81 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamewasili nchini Guinea, kwa lengo la kusaidia kukabiliana na janga la Ebola.

Timu hiyo ya wafanyakazi 81 inahusisha madaktari, wauguzi, wataalam wa maabara, saikolojia na wataalam wa mawasiliano, huku taarifa zikisema kwamba wataalam hao wataanza kazi moja kwa moja katika vitengo husika na kutibu ugonjwa wa Ebola nchini Guinea.

Mbali na hayo inaelezwa kuwa wataalam hao watatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya wa mitaa ya nchi hiyo kuhusu namna ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Ebola nchini humo.

Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa takwimu mpya za mlipuko wa Ebola, ambapo vifo vilivyotokana na Ebola katika nchi tatu zilizoathirika zaidi imepita watu 8,000.

Takwimu hizo mpya ni kwa nchi za Sierra Leone, Guinea na Liberia pekee, ambapo watu 8,153 wameripotiwa kufa, huku watu 20, 656 wakiwa wameugua ugonjwa huo katika nchi hizo tatu.

Aidha, takwimu hizo zinaonesha kuwa Sierra Leone imekuwa na wagonjwa 9,772 na vifo 2,915 na Liberia imekuwa na wagonjwa 8,115 na vifo 3471, halikadhalika Guinea imeripotiwa kuwa na wagonjwa 2,769 na vifo 1,767.

Kwa ujumla takwimu hizo ni hadi kufikia Disemba 31 kwa upande wa Liberia, na kwa upande wa nchi za Sierra Leone na Guinea takwimu hizo ni hadi Januari 3, 2015.

Mbali na hayo, pia nchini Mali kumekuwepo na taarifa za wagonjwa 8 na vifo vya watu 6. Ambapo Uingereza ina mgonjwa mmoja na hakuna kifo.
Unastahili kupata habari zote rafiki na kama wewe ni mtu wa kupenda habari basi ni vyema ukaendelea kuwa nasi kila iitwapo leo, tunathamini sana uwepo wako msomaji wetu.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname