KUSHUKA KWA GHARAMA ZA MAFUTA INAWEZA KUWA NI MWELEKEO WA UCHUMI DUNI KWA MWAKA HUU



MKUU wa shirika la fedha la kimataifa IMF, Christine Lagarde amesema kushuka kwa bei za mafuta na kuimarika kwa uchumi wa Marekani havitatosha kuboresha mwelekeo wa uchumi wa dunia mwaka huu wa 2015.

Lagarde alisema wakati mafuta ya bei nafuu yatasaidia watumiaji katika sehemu nyingi za dunia, Marekani ndiyo itakayo kuwa nchi pekee yenye uchumi mkubwa itakayoepukana na udhaifu katika sekta ya uwekezaji na ununuzi.

Katika hotuba inayoangazia ripoti ya IMF kuhusu matarajio ya uchumi wa dunia, inayotarajiwa kutolewa wiki ijayo, Lagarde alisema kanda inayotumia sarafu ya euro na Japan zipo katika hatari ya kuingia katika kipindi cha muda mrefu cha ukuaji dhaifu na mfumuko hatari wa bei.

"Maswali ya wazi tuliyonayo wakati huu ni je, kushuka kwa bei za mafuta na uchumi imara nchini Marekani vitupe matumaini kuhusu uchumi wa dunia? Jibu ni hapana, hapana, hapana, kwa nini? Kwa sababu kuna masuala chungu mzima, athari za mgogoro wa kiuchumi ambazo bado tunazo, na ambazo zinadhoofisha uchumi wetu," alisema Lagarde katika hotuba yake kwa baraza la masuala ya kigeni la Marekani.
Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
Hata hivyo, Lagarde alisema kupungua kwa bei za mafuta ni jambo zuri sana kwa uchumi wa dunia, lakini uchumi huo uko katika hali mbaya sana, na hilo halitasaidia, na kuongeza kuwa kupungua kwa bei ya mafuta kunasaidia kupandisha uwezo wa wananchi kununua bidhaa na kunaongeza mahitaji binafsi ya mafuta katika mataifa yanayonunua kutoka nje, na kutegemea ni kwa muda gani bei zitaendelea kuwa chini, hili linaweza kutoa mchango katika ukuaji wa uchimi wa dunia kwa muda.

Mbali na hayo alieleza kuwa kuimarika kwa uchumi wa Marekani pia kunaelekea kuwa maumivu kwa baadhi ya mataifa. Wakati taarifa za Marekani kutoka Disemba zimewasukuma wawekezaji kuamini kuwa benki kuu ya nchi hiyo itasubiri pengine hadi mwezi Oktoba kupandisha viwango vya riba, Lagarde alisema kukazwa kwa sera ya fedha kunakotarajiwa kunaweza kuvuruga masoko ya fedha, hasa katika mataifa masikini zaidi ambako mabenki na makampuni yamekopa dola zaidi katika miaka ya karibuni.

Naye Rais wa Benki Kuu ya Ulaya ECB, Mario Draghi, amesema benki hiyo imeyaanda masoko ya fedha kwa ununuzi wa dhamana kubwa za fedha ili kukabiliana na kuongezeka kwa fedha katika mzunguko.

Source: DW

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname