MADAM RITA:BONGO STAR SEARCH HAIJAFA


Kufuatia kutokuwepo kwa shindano la Bongo Star Search kwa mwaka jana na kusababisha baadhi ya mashabiki kudhani kwamba huenda mashindano hayo yamekufa, hatimaye Mkurugenzi wa Benchmark na Jaji Mkuu wa shindano hilo Rita Poulsen amewataka mashabiki wa shindano hilo kuondoa hofu.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Rita alisema kuwa pamoja na kuchelewa kuanza katika msimu huu, shindano hilo litafanyika na kwamba mipango inakamilishwa.

Kuna mambo tunayaweka sawa, hadi mwishoni mwa mwezi Februari mipango itakuwa imekamilika,” alisema Rita.

Jaji huyo ambaye ni maarufu kwa jina la Madam Rita alisema amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa wadau na wapenzi wa mashindano hayo wakihoji kuhusu kuchelewa kuanza kwa msimu mpya wa BSS.

Aidha, madam Rita alisema kuwa kuanza kwa msimu huo mpya kutakwenda sambamba na udhamini mpya, huku akibainisha kwamba udhamini wa awali wa Kampuni ya Zantel kwa BSS umekwisha muda wake na msimu mpya utakuwa na wadhamini wapya ambapo tayari kampuni mbalimbali zimeomba kudhamini shindano hilo ambalo hujumisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali nchini na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki.

Pamoja na hayo, kuhusu majaji Madam Rita alisema yeye atabaki kuwa jaji kiongozi akiwa na Master J sambamba na Salama Jabir.

Mbali na hayo, Ritha alisema, licha ya kutafuta vipaji mikoani pia wamekuwa wakitoa elimu ya vijana kujitambua na athari za magonjwa mbalimbali ikiwamo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Shindano hilo lilianza mwaka 2006 kwa kusaka vipaji vya vijana wa Kitanzania na kufanikiwa kuibua vipaji mbalimbali vya wasanii huku baadhi yso wakiendelea kufanya vizuri. Baadhi ya wasanii waliotambulika kupitia BSS na wanaendelea kufanya vizuri ni pamoja na Kala Jeremiah, Peter Msechu, Walter Chilambo, Baby Madaha na Meninah.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname