Abiria zaidi ya arobaini wamenusurika kifo baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka mjini Tabora kuelekea kata ya Goweko wilayani Uyui mkoani humo kuligonga gari la mizigo, huku chanzo cha ajali hiyo kikielezwa kuwa basi hilo kutokuwa na breki hivyo kuchangia ajali hiyo.
Wakizungumza na ITV abiria waliokuwa katika basi hilo aina ya Scania la kampuni ya Ladak lenye namba za usajili T 918 ACG, wamesema kuwa, kutokana na mwendo wa gari hilo dereva ambaye hakujulikana jina lake mara moja, alishindwa kulimudu na kusababisha kuligonga gari la mizigo aina ya Scania lenye namba za usajili T 699 ABN.
Akizungumzia ajali hiyo kwa njia ya simu Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani Tabora mratibu wa polisi Bw. Michael Dereli amesema ajali hiyo haikuwa na madhara kwa abiria, lakini katika wiki hii ya usalama barabarani watahakikisha wanatatua changamoto ya magari kama hayo ambayo hayakidhi matakwa ya kusafirisha abiria.
No comments:
Post a Comment