MAALIM SEIF ASEMA HATAMBUI KUHUSU KURUDIWA KWA UCHAGUZI WA ZNZ NA HAWATAKUBALI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) na aliyekuwa mgombea urais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar  Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa hana taarifa zozote juu ya swala la kurudiwa kwa uchaguzi na badala yake amehitaji kura zilizobaki zihesabiwe na mshindi aweze kutangazwa.

Akizungumza leo na waandishi wa habari katika hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar kama inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), haina msingi, haikubaliki na sio halali kikatiba.

“Hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa kisheria. Sidhani kama tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif.

Makamu huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameeleza kuwa tayari wameshafanya vikao nane vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar lakini hawakukubaliana kurudia uchaguzi kama baadhi ya viongozi wa CCM walivyoeleza.

Aidha, Maalim Seif amekanusha kilichoelezwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd baada ya kukutana na Rais John Magufuli, kuwa rais alisema warudie Zanzibar kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema hivyo alipokutana naye.

Maalim Seif amemtaka Rais Dkt John Magufuli kuingilia kati suala hilo katika kuweza kupata suluhu ya mwafaka kwa amani kutokana na Dk Ali Mohamed kushindwa kuhimili mazungumzo hayo.

Seif pia amesema kuwa endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo hautawezekana.

Mbali na hayo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu kwa kutoa tamko lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu hiyo kikatiba.

Pia ameitaka ZEC iongozwe na makamu mwenyekiti wake kwa mujibu wa katiba pamoja na wajumbe wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi.

Pamoja na hayo Maalim Seif ameeleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa nguvu marudio ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na chama chake hawatakubali.

No comments:

Post a Comment

Ad Inside Post

Comments system

Disqus Shortname